Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kumekucha Yanga, Ramovic ataja usajili wake

Yanga Pict
Yanga Pict

Muktasari:

  • Pamoja na kusaka ushindi wa kwanza tangu ajiunge na Yanga siku chache zilizopita, kocha wa Sead Ramovic anafikiria kufanya kitu kwenye dirisha dogo la Krismasi ili kubadili upepo wa matokeo na kurejesha hadhi ya timu.

YANGA inacheza na Namungo Jumamosi hii kwenye mechi ya ligi. Licha ya kwamba imekuwa na matokeo mabovu hivi karibuni, lakini haikuwahi kupoteza kwa Namungo katika mechi ya ligi zaidi ya sare tatu na kushinda michezo mitano.

Pamoja na kusaka ushindi wa kwanza tangu ajiunge na Yanga siku chache zilizopita, kocha wa Sead Ramovic anafikiria kufanya kitu kwenye dirisha dogo la Krismasi ili kubadili upepo wa matokeo na kurejesha hadhi ya timu.

Mwanaspoti linajua kwamba mezani kwa mabosi wa Yanga kuna mahitaji mawili ya Ramovic. Lakini mmoja kati ya hao ni wa haraka sana ikiwezekana hata kesho kama kuna sehemu yuko tayari atue mazoezini ili aweze kuweka hesabu sawa.

Kocha ameshtukia kwamba kwenye ukuta anahitaji beki wa kati haraka atakayepangua au kuziba kwa ujazo uleule kwa mabeki wanaocheza sasa nahodha msaidizi Dickson Job na Ibrahim Abdulah ‘Bacca’.

Tathimini yake ni kwamba wakati huu nahodha mkuu beki Bakari Mwamnyeto anajitafuta wanahitaji beki eneo hilo haraka ili kuipa timu  utulivu endapo kati ya Job na Bacca wakikosekana. Mbali na hilo pia kocha huyo amewaambia viongozi ni vigumu kwa mabeki hao kupumzishwa kwa kuwa hakuna uhakika sana kwa wale wanaosubiri nje wanaoweza kucheza kwa ubora uleule.

“Kocha anasema mzunguko wa kuwatumia wachezaji wake utakuwa mkubwa, lakini kwasasa utawezaje kumpumzisha Bacca au Job wakati huna uhakika sana ya wale waliokuwa nje,” alidokeza mmoja wa mabosi wa usajili wa Yanga.

“Anasema Mwamnyeto ni beki mzuri lakini anahitaji muda kumuangalia kama anaweza kubadilika kuja juu kucheza kwa ushindani mkubwa lakini hata kama itashindikana bado anahitaji beki mwenye ubora wa Job na Bacca.”

Yanga itamkosa Bacca leo hatua itakayowafanya makocha kulazimika kumpa nafasi Mwamnyeto ambaye ndiye beki pekee aliye tayari kutumiwa eneo hilo baada ya kuumia kwa kiungo mkabaji Aziz Adambwile ambaye alikuwa anatumiwa kucheza eneo hilo ba kocha aliyepita Miguel Gamondi.

Mwanaspoti linajua kabla Ramovic hajatua kuna kitu kilikuwa kinaendelea kati ya beki wa Coastal Union, Lameck Lawi na Yanga ambapo kocha huyo amepewa jina la mchezaji huyo na kuonyeshwa baadhi ya video zake.

Lakini Mwanaspoti linajua amewajibu viongozi anahitaji kumuona uso kwa uso akicheza mechi iwe yeye au mmoja wasaidizi wake atakayemtuma.


PALE MBELE

Mbali na beki wa kati kocha huyo anaumiza kichwa kujiridhisha juu ya ufanisi wa washambuliaji wawili walio tayari, Prince Dube na Jean Baleke wakati Clement Mzize akiendelea kuwa nje kufuatia kuumia akiwa Stars.

Ramovic hajaelewa sawasawa kiwango cha Dube, lakini pia Baleke ambaye kwenye mchezo uliopita aliendelea kutupwa jukwaani kama ilivyokuwa kwa Miguel Gamondi.

Mwanaspoti linajua Yanga inamfikiria pia straika Bayo Aziz Fahad wa Uganda Cranes. Sifa kubwa ya Bayo inatajwa ni kufunga mabao ya vichwa akitumia vyema kimo chake cha futi 6 inchi 6 na pia anasifika kwa mashuti makali anapojongea kwenye lango la timu pinzani. Kwa sasa, Bayo ni mchezaji huru baada ya kuachana na MFK Vyskov inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Czech ambayo aliichezea mechi 42 na kuifungia mabao manane.

Kabla ya kujiunga na Vyskov, Bayo aliitumikia Ashdod inayoshiriki Ligi Kuu ya Israel ambako katika mechi 41 alizoichezea, alifunga mabao manane huku akipiga pasi moja ya mwisho. Katika timu ya taifa ya Uganda, mshambuliaji huyo amecheza mechi 21 na kuhusika na mabao tisa, akifunga mabao manane (8) na kupiga pasi moja ya mwisho. Ni mchezaji mwenye uzoefu kutokana na idadi ya klabu alizowahi kuzichezea ndani ya nje ya Afrika ambazo ni MFK Vyskov (Czech), FC Ashdod (Israel), Bnei Sakhnin (Israel), Buildcon FC (Zambia), Vipers (Uganda) na Proline (Uganda).

Dirisha dogo la usajili linafunguliwa Desemba 15 na kufungwa Januari 15.