Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kumekucha Serengeti Marathon

ZAIDI ya watu 500 kutoka ndani na nje wanatarajiwa kushiriki mbio za marathon zijulikanazo kama Serengeti Migration Marathon 2020 mbio ambazo zinatarajiwa kufanyika Septemba 6 mwaka huu wilayani Serengeti.

Mbio hizo mbali na kutangaza utalii pia  zinatarajiwa kuleta fursa za kiuchumi kwa wakazi wa mji wa Mugumu na wilaya ya Serengeti pamoja na mkoa wa Mara kwa ujumla kutokana na idadi kubwa ya watu wanaotarajiwa kushirki tukio hilo linaloandaliwa na taasisi ya Serengeti Tourism Sports Agency (SETSA).

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Geofrey Werema lengo kuu ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu uhifadhi endelevu sambamba na kutangaza utalii  kutokana na umuhimu wa ikolojia ya Serengeti kwa maendeleo ya sekta ya utalii na nchi kwa ujumla.

Anasema kuwa mbio hizo zimeasisiwa kutokana na mambo mbalimbali yanayopatikana ndani ya uoto wa Serengeti ikiwemo hifadhi bora duniani yenye maajabu kadhaa likiwemo tukio kubwa la kila mwaka linalohusisha uhamiaji wa wanyama aina ya Nyumbu wanaoambatana na wanyama wengine kama vile Pundamilia kutoka Kusini mwa hifadhi hiyo kuelekea Masai Mara Kenya.

Anasema kuwa kutokana na  ukweli kwamba eneo hilo limekuwa kivutio kikuu cha watalii kutoka ndani na nje ya nchi lakini linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro kati ya binadamu na wanyama hasa ikizingatiwa kuwa zipo shughuli za kibindamu zinazofanywa na wakazi wanaozunguka hifadhi hiyo shughuli ambazo sio rafiki kwa ikolojia ya Serengeti na uhifadhi kwa ujumla.

Anasema kuwa kubwa zaidi binadamu wamekuwa wakijiingiza katika vitendo vya ujangili kwaajili ya kupata kitoweo sambamba na kujipatia kipato jambo ambalo limekuwa likitishia uhai wa uendelevu na uwepo wa moja ya maajabu hayo ya dunia.

Werema anasema kuwa hapo ndipo yeye pamoja na wenzake watatu ambao ni wazawa wa wilaya ya Serengeti walipoona kuwa wana wajibu wa kutoa mchango wao katika uhifadhi endelevu wa hifadhi hiyo muhimu kwa maendeleo ya Taifa na ndipo walipokuja na wazo la Serengeti Migration Marathon.

Anasema kuwa wazo hilo liliwapelekea kusajili tukio hilo katika mamlaka  husika yaani Chama cha Riadha nchini (RT) hivyo tukio hilo litakuwa endelevu ambapo litakuwa likifanyika kila Jumapili ya kwanza ya Septemba ambapo lengo likiwa ni kushiriki katika kuhifadhi Serengeti kupitia michezo   (mbio).

 

Anasema kuwa katika tukio hilo kutakuwepo na vivutio kama fursa ya kutembelea hifadhi ya Serengeti na mbio mbalimbali kama mbio za nusu marathon za kilomita 21, mbio za kilomita 10 pamoja na mbio za familia za kilomita 5.2 na kwamba tukio hilo limepangwa kufanyika mjini Mugumu ambapo ndipo walipo walengwa wakuu wa  uhifadhi wa Serengeti.

Katika matukio hayo kutakuwa na ujumbe unaolenga kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa uhifadhi endelevu pamoja na madhara ya ujangili katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti na nini kifanyike ili kuondokana na changamoto hizo na hatimaye ikolojia ya Serengeti iweze kutumika vema katika kutangaza utalii kwa maendeleo ya wakazi wa Serengeti na Taifa kwa ujumla.

Wakizungumzia tukuo hilo baadhi ya wakazi wa mkoa wa Mara wamesema kuwa tukio limekuja muda muafaka na eneo muafaka na kwamba wanaamini kuwa litakuwa na faida kiuchumi na kijamii.

Musa John anasema kuwa kwa muda mrefu shughuli nyingi zinazohusu Serengeti zimekuwa zikifanyika nje ya mkoa wa Mara hivyo kupoteza maana halisi ya shughuli hizo na kwamba waandaaji wanastahili pongezi kwa kuamua kufanya tukio hilo katika eneo husika.

"Kama utakumbuka baada ya Serengeti kutangazwa kuwa hifadhi bora shughuli za kupokea tuzo zilifanyikia Arusha ila tunashukuru kwa juhudi za mkuu  wetu wa Mkoa, Adam Malima  alipambana mpaka sherehe hizo kwa mara ya pili zilifanyika mkoani kwetu " anasema Musa.

Musa anaongeza kuwa matukio mengi yanayohusu hifadhi ya Serengeti na uendelevu wake yakiwa yanafanyika ndani ya Serengeti anaamini kuwa matukio kama ujangili yatapungua kwa kiasi kikubwa kwavile watu watakuwa na uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa hifadhi hiyo kwa maendeleo yao.

Lydia Manyama mbali na kuwapongeza wandaaji wa tukio hilo lakini pia anatoa wito kwa wadau wegine kubuni vitu mbalimbali ambavyo vitaamsha ari ya wakazi wa wilaya ya Serengeti na mkoa wa Mara kuona umuhimu wa kushiriki katika kutunza ikolojia ya Serengeti.

Anasema kuwa anaamini kuwa mbio hizo zitakuwa endelevu na kwamba zitakuwa na mchango mkubwa katika kukuza utalii mkoani Mara hivyo kuendelea kutoa wito kwa mashirika na makampuni mbalimbali waweze kushirikiana na waandaaji ili ziweze kuwa kubwa zaidi na zenye mafanikio.

Anasema kuwa mbio hizo zitakuwa ni nembo ya mkoa wa Mara hasa ikizingatiwa kuwa eneo kubwa la hifadhi ya Taifa ya Serengeti inapatikana ndani ya mkoa huo ambapo pia amewaomba watu mbalimbali kujitokeza kushiriki mbio hizo.

Makilagi John anasema matukio kama haya hayana budi kuandaliwa mara kwa mara kwani mbali na kuwa na umuhimu katika uhifadhi lakini yanasaidia kukuza uchumi wa eneo hilo ambalo kwa miaka mingi limesahaulika ingawa lina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.