Kumbe usajili ndiyo unakwamisha mkutano

Mashabiki wa Simba.
Muktasari:
- Simba bado hawajakamilisha wachezaji wa kigeni ambao ni Janvier Besala Bokungu (DR Congo), Blagnon Goue Frederick (Ivory Coast) ambao kocha wao Joseph Omog amesema wasipewe mikataba mpaka wafanyiwe majaribio pamoja na Laudit Mavugo (Burundi) ambaye anaonekana kuwasumbua.
SABABU mbili za kuahirishwa kwa mkutano mkuu wa klabu ya Simba zimetajwa kuwa ni wanachama wengi kutolipa ada zao za mwaka pamoja na kusubiri usajili wa wachezaji wa kigeni ukamilike.
Simba bado hawajakamilisha wachezaji wa kigeni ambao ni Janvier Besala Bokungu (DR Congo), Blagnon Goue Frederick (Ivory Coast) ambao kocha wao Joseph Omog amesema wasipewe mikataba mpaka wafanyiwe majaribio pamoja na Laudit Mavugo (Burundi) ambaye anaonekana kuwasumbua.
Usajili wa Shiza Kichuya bado haujakamilika huku Hassan Kabunda akiwatosa kabisa ila wamemalizana na Mohamed Ibrahim, Mdhamiru Yassin, Hamad Juma na Jamal Mnyate.
Awali mkutano huo wa kila mwaka ulipangwa kufanyika Julai 10, Jumapili umeelezwa kusogezwa mbele hadi Julai 31 ambapo utajadili mambo mbalimbali ya maendeleo ya klabu hiyo pamoja na kupanga mipango yao ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Mkutano huo ambao pia umekuwa ukitajwa kufanyika tangu mwanzoni mwa mwaka huu lakini haikufanyika kutokana na klabu hiyo kuwa kwenye mpambano mkali wa kupigania timu yao ishike nafasi bora za juu msimu wa ligi uliopita ingawa walimaliza wakiwa nafasi ya tatu wakiongozwa na Mabingwa mara mbili mfululizo, Yanga pamoja na Azam waliomaliza nafasi ya pili.
Mwanaspoti ilizungumza na Wenyeviti mbalimbali wa matawi ya Simba, ambapo walisema hoja iliyotolewa na viongozi wao ya kuiandaa timu ili iende kambini haina mashiko makubwa kwani hakuna uhusiano wowote na mkutano wa wanachama huku wakisisitiza wanachama ambao hawajalipa ada walipe.
Mwenyekiti wa Wilaya ya Kinondoni, Omary Masirahi alisema kuwa “Watu wengi ni wavivu wa kulipa ada, huwa tunalipa kwa matukio maalumu, huu mkutano ni haki yao lakini utaendeshwaji kama hawalipi ada? Zilipwe ada mkutano ufanyike kwa kuhudhuriwa na wanachama wengi. Kila mwanachama ana haki ya kupewa taarifa wakiwa wachache baadhi yao hawatajua nini kimejadiliwa.”
“Naamini mpaka kufika muda ambao viongozi wamesogeza wengi watakuwa wamelipa na uhudhuliaji utakuwa mkubwa ambapo tutaweza kujadili mambo yetu kwa upana mkubwa ikiwa ni pamoja na kupata mawazo tofauti,” alisema Masirahi
Naye Mwenyekiti wa tawi la Simba Dume la Temboni, Ben Shija alisema: “Viongozi wana sababu zao nyuma ya pazia, naamini mkutano huu ungefanyika pasingekalika, watu wanataka kusikia mambo ya maana, usajili haueleweki halafu wanasema wanafanya kisayansi, kusogeza mkutano mbele kwa kigezo cha kuandaa timu kwanza hiyo sio sababu.
“Wameishaona wameharibu, njia pekee ni kuweka mambo yao sawa, tumesikia usajili wa wachezaji wengi tu Simba sasa wako wapi? Kuandaa timu ni jambo jema ila halizuii mkutano kufanyika. Kuhusu ulipaji wa ada miaka yote iko hivyo kwamba wanachama wana tatizo la kulipa ada mara nyingi wanalipa siku ya mkutano, pia wanapaswa kuwa na msimamo mwanachama asiyelipa hana haki ya kushiriki,” alisema Shija
Mwenyekiti wa Tawi la Mpira Pesa, Ustadh Masoud alisema “Wanachama wa Simba tumezoea kulipa ada hata kwenye mambo muhimu kama haya, wanachama tunapaswa kulipa ada zetu huu ni mkutano mkuu na sio uchaguzi, naamini wanachama wengi hawalipi ada mpaka wakati wa uchaguzi ili walipiwe, hilo sio jambo jema, tulipe ada ili tuwe wengi kujadili mambo ya maendeleo ya Simba.”
“Suala la usajili lina uzito wake, mkutano ukifanyika viongozi wangetupa taarifa gani ya usajili maana tunaona mambo bado, hivyo nadhani wanataka wakamilishe kwanza hilo ili waje kutupa taarifa iliyokamilika,” alisema Ustadh.