Kumbe Nabi alimkataa Makambo
Kocha wa Yanga Nesreddine Nabi amesharejea nchini na Mwanaspoti linafahamu Mtunisia huyo hakutaka kumsajili Makambo, lakini mabosi wa Yanga tayari walishafika mbali katika kumrejesha.
Kitu rahisi kwa mabosi wa Yanga ni kwamba karibu mashabiki na wanachama wengi waliona ni bora Makambo arejeshwe na wao kuamua kusimamia msimamo huo wa wafuasi wao.
Nabi hakuvutiwa na rekodi ya Makambo akiwa na Horoya kwani alishindwa kutamba na kuamua kusitisha mkataba wake na sasa anarejea Jangwani.
Mapema Makambo aliliambia Mwanaspoti kwamba anarejea Yanga kuendeleza kazi akianzia palepale alipoishia.
“Mimi Tanzania ni nyumbani kwangu kwa pili na Yanga ni klabu yangu, nikirudi nakuja kuendelea pale nilipoishia,” alisema Makambo wiki moja iliyopita.
Mshambuliaji huyo anayeshikilia rekodi ya kuwa straika aliyeifungua Yanga mabao mengi ndani ya misimu minne iliyopita, atasaini mkataba wa miaka miwili utakaombana kutakiwa kuonyesha makali katika mwaka wake wa kwanza na mara baada ya kusaini mkataba huo anarejea kwao DR Congo ambako anakwenda kumalizia harakati za kuoa.