Kumbe Mkata Umeme anawainjoi tu

Justine Zulu
Muktasari:
Kumbe anajua ni yeye Mkata Umeme? “Mwanzoni sikujua kama mkata umeme ni mimi, niliwahi kulisikia jina hilo kwa wachezaji wenzangu wakilitaja siku moja tukiwa mazoezini ndipo likatajwa tena wachezaji wenzangu wakacheka na kuanza kunitania, Mkata Umeme.”
KIUNGO Mzambia, Justine Zulu maarufu kama Mkata Umeme amekuwa mchezaji wa kwanza kutoka benchi kujihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza cha Yanga huku akiwaacha mastaa wengine wanane wakizipigania nafasi zao.
Kumbe anajua ni yeye Mkata Umeme? “Mwanzoni sikujua kama mkata umeme ni mimi, niliwahi kulisikia jina hilo kwa wachezaji wenzangu wakilitaja siku moja tukiwa mazoezini ndipo likatajwa tena wachezaji wenzangu wakacheka na kuanza kunitania, Mkata Umeme.”
“Sikutaka huo utani, nikafuatilia na kubaini maana ya jina hilo, kwa kweli nilicheka sana ingawa pia nililipenda kwani nilijua nimepewa kutokana na kiwango changu lakini pia kwa kuwa nimetokea Zesco,” alisema Zulu huku akicheka.
Alisema hakushangazwa sana na jina hilo kwani katika soka hivyo ni vitu vya kawaida kwa mashabiki kumpachika mchezaji jina na likavuma kuliko jina lake halisi huku akiahidi kulitendea haki jina hilo kwa kuitumikia Yanga kwa nguvu zake zote.
Zulu alitua Yanga katika usajili wa dirisha dogo na kuanza kusugua benchi ambapo Yanga ilianza kumtumia kiungo, Said Juma ‘Makapu’ kama kiungo wa chini lakini sasa mambo yameanza kubadilika.
Kuingia kwa Zulu katika kikosi cha kwanza kunakuja siku chache baada ya mshambuliaji, Emmanuel Martin aliyejiunga na Yanga akitokea JKU ya visiwani hapa kumng’oa Deus Kaseke katika kikosi hicho jambo ambalo limewashtua wengi.
Kaseke alikuwa winga wa kushoto wa kudumu katika kikosi hicho cha Yanga lakini ameukubali muziki wa Martin na kukubali kusugua benchi lakini sasa Zulu naye amemrudisha Makapu katika benchi.
Zulu amewaacha wachezaji Hassan Kessy, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Makapu, Geofrey Mwashiuya, Juma Mahadhi, Kaseke, Oscar Joshua, Matteo Antony na Yusuf Mhilu wakiendelea kupambana kutafuta maisha ya kudumu kikosini hapo.
MWAMBUSI ANENA
“Alipojiunga na timu hakuwa fiti, tumekuja hapa na tumeona ni vizuri tukaanza kumpa nafasi ili aweze kuwa fiti zaidi. Nadhani mpaka sasa ameanza kuonyesha uwezo mzuri, mpaka mashindano yanakwisha atakuwa mtu mwingine kabisa kikosini,” alisema Mwambusi.
“Hata Martin (Emmanuel) naye amekuwa makini, anajitahidi kuingia katika mfumo wetu taratibu, naamini bado ana vitu vingi vya kutuonyesha,” alifafanua Mkufunzi huyo wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf).