KUFUNGIWA VIWANJA NI MASWALI NA MAJIBU YANAYOACHA MASWALI

SEPTEMBA 6, 2020, msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2020/21 ulianza rasmi ambapo mpaka sasa kila timu imecheza mechi tano.

Baada ya mechi hizo, ligi itasimama kupisha mechi ya kirafiki ya timu ya Taifa ‘Taifa’ ambayo ipo kwenye kalenda ya Shirisho la Soka duniani (Fifa) itakayochezwa Oktoba 11 dhidi ya Burundi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Lakini tangu kuanza kwa ligi kasoro kubwa mpaka sasa ni kufungwa kwa viwanja vitano ikiwa ni mapema tangu ligi hiyo ianze.

Hivi sasa hakuna malalamiko ya waamuzi yaliyopigiwa kelele kama ilivyozoweleka ambapo inaonyesha kamati inayosimamia waamuzi imeboreshwa na inasimimia misingi ya kazi.

Tatizo sasa limehamia kwenye viwanja ambapo ndio kwanza ligi bado mbichi, lakini vitano vimefungwa kwa kukosa sifa ambavyo ni Gwambina (Misungwi), Karume (Musoma), Ushirika (Moshi), Mabatini (Pwani) na Jamhuri (Morogoro).

Mwanaspoti limefanya uchunguzi ambapo limebaini kuwapo kwa baadhi ya viwanja havikukaguliwa kabla ya ligi kuanza. Gazeti hili limezungumza na pande zote baada ya kubaini baadhi ya mambo yaliyochangia viwanja hivyo kufungiwa ambao ni mameneja wa viwanja, viongozi wa timu, Bodi ya Ligi (TPLB), Kamati ya Leseni yenye jukumu hilo na Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Mbali na hao, pia wataalamu wa afya wamezungumzia madhara ambayo wanaweza kuyapata wachezaji na wote wanaoingia kwenye viwanja hivyo kushuhudia mechi.

KARUME - MUSOMA

Mwenyekiti wa Biashara United, Seleman Mataso anasema marekebisho ya Uwanja wa Karume - Mara yamefikia hatua nzuri na wanategemea wataanza kuutumia ndani ya muda mfupi ujao ambapo ulifungwa kwa siku 21.

“Tulitenga muda wa siku 21 kufanya ukarabati maeneo tuliyoagizwa na Bodi ya Ligi na TFF na hadi sasa umefikia takribani asilimia 90, na ndani ya siku chache zijazo utakuwa umekamilika.

“Ukikamilika tutawaandikia barua Shirikisho (TFF) na Bodi kuwajulisha ili waje kufanya ukaguzi kuona kama utastahili tuendelee kuutumia au la,” anasema Mataso.

MABATINI - PWANI

Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire anasema kufungiwa kwa uwanja wao wa nyumbani uliopo Mlandizi umewapa athari mbili kubwa.

“Kwanza mashabiki wanakosa fursa ya kuiona timu, kuipa sapoti na kushirikiana masuala mbalimbali yanayohusu timu yao, lakini jambo la pili, gharama za kucheza nje ya hapa ni kubwa kwa maana ya hoteli na usafiri.

“Mtazamo wangu, kamati na mamlaka husika ziwe zinafanya ukaguzi na kutoa uamuzi mapema ili kama kuna tofauti zirekebishwe. Pamoja na yote kuonyesha utii kwa mamlaka tumeanza kuchukua hatua za kufanyia kazi marekebisho ambayo wametuelekeza.

“Tutaongeza idadi ya vyoo licha ya sasa uwanja wetu kuwa na vyoo vizuri viwili na vyenye matundu nane kama ilivyo kwa viwanja vya Benjamin Mkapa, Uhuru na Azam Complex, pia tunaendelea kuboresha vyumba vya kubadilishia nguo. Tunarekebisha pia eneo la kuchezea na sehemu ya kukaa makocha na wachezaji wa akiba,” anasema.

MANUNGU, JAMHURI, GAIRO - MOROGORO

Ofisa wa Sheria na Utawala wa Mtibwa Sugar, Swabri Abubakar anasema kuwa uamuzi wa kuufungia Uwanja wa Jamhuri ni pigo kwao.

“Kiukweli hili ni pigo kwetu kuanzia uwanjani. Faida ya kucheza nyumbani tunaikosa kabisa tutalazimika kucheza nje ya Morogoro na kuwakosa mashabiki wetu wanaotupa nguvu,” anasema.
“Pili kuzoea hali ya hewa ya sehemu ni utakapochagua kwa mfano Gairo ilikuwa sehemu yenye baridi sana na tulianza kuzoea.

Tutajitahidi kuuboresha Uwanja wa Jamhuri, lakini mipango yetu ni kujenga uwanja wetu wa nyumbani mwingine tofauti na ule wa awali,” anasema.

Hata hivyo inaelezwa kuwa Uwanja wa Jamhuri, tatizo lililopo ni eneo la kuchezea ambapo marekebisho yake sio makubwa sana.

Kilichoonekana kwenye uwanja huo ni kuwa mkavu sana ambapo unaweza kusababisha majeraha kwa wachezaji.

USHIRIKA - MOSHI (Haukukaguliwa)

Kwa mujibu wa maelezo ya Meneja wa Uwanja wa Ushirika, Jafary Kiango uwanja huo haukukaguliwa kabisa.

Kiango anasema kabla ya ligi kuanza hakukuwa na ugeni kutoka Bodi ya Ligi wala Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuukagua uwanja ndio maana walifanya maandalizi ambayo waliamini upo sawa.

Kiango anasema baada ya kucheza mechi na Namungo ndipo walipopokea barua kutoka TPLB kuwa wanahitajika kufanya marekebisho ya uwanja hasa eneo la kuchezea.

“Kwa maana hiyo siku chache mara baada ya kupokea barua uongozi wa Chuo cha Ushirika na Polisi Tanzania walikutana ili kujadili na kuona namna gani wanafanya marekebisho ili mechi ziendelee kuchezwa uwanja huo,” anasema. “Nakumbuka Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred

Kidau alipita siku moja hapa Ushirika kufungua mafunzo ya watoto ndio alitueleza tunatakiwa kuboresha uwanja, nasi tukafanya kwa uwezo tuliokuwa nao mpaka kutumika katika ligi, lakini mara baada ya mechi tulipokea barua ya kufungiwa,” anasema Kiango.

GWAMBINA - MISUNGWI

Uwanja wa Gwambina ndio ulikuwa wa kwanza kufungiwa na TPLB baada ya timu hiyo kucheza mechi moja. Bodi iliufunga ikiwa ni muda mfupi tu tangu mechi imalizike.

Sababu kubwa ya kuufunga uwanja huo ilikuwa eneo la kuchezea kutokidhi vigezo ingawa nao ulikaguliwa na Kamati ya Leseni kabla ya ligi kuanza. Maswali mengi yaliibuka baada ya kuufungia ambapo Meneja wa uwanja huo, Mohammed Ngaiza anakiri kwamba haukustahili kwa matumizi ya mechi.

“Ligi iliporuhusiwa kuendelea baada ya katazo la mikusanyiko wakati wa corona tuliporejea ulikuwa ni muda mfupi sana wa kufanya marekebisho. Ligi ilipomalizika tuliamua kuufanyia marekebisho, lakini ilikuwa ni muda mfupi wa mapumziko na Ligi Kuu kuanza kwani sehemu ambayo ilikuwa imeharibika tulijaza vifusi vya udongo ambapo tuliona tukimwagilia sana maji basi tutauharibu kwani utakuwa na matope,” anasema Ngaiza.

“Tumefanya marekebisho na upande wetu tunaona tumemaliza na upo tayari kwa matumizi ingawa tulipofungiwa hatukupewa muda, tumetoa taarifa TFF juu ya kukamilisha hivyo tunawasubiri wao kuja kuukagua na kutupa mwongozo mwingine.”

TPLB

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo ambao ndio walivifungia viwanja hivyo, hakuwa tayari kuelezea juu ya ukaguzi uliofanywa kabla ya ligi kuanza.

“Kuna kamati inayoshughulikia mambo ya kukagua viwanja, hiyo ndio yenye mamlaka ya kuzungumzia hili, kazi yangu kubwa ni kuhakikisha mpira unachezwa uwanja mzuri, tunaendelea kufuatilia viwanja vingine,” anasema.

“Nikijiridhisha naruhusu kuchezwa, nikiona haukidhi unafungiwa, hivyo tutaendelea kufanya hivyo haijarishi ulikaguliwa ama haukukaguliwa, masuala hayo wanajua wenyewe, mpira ni mchezo wa wazi ambao unachezwa kwenye viwanja vinavyoonekana.

“Wenye viwanja pamoja na watumiaji ambao ni timu wanafahamu vizuri na wana uwezo wa kurekebisha viwanja vyao kuwa kwenye ubora, hivyo wakifungiwa watarekebisha tu.”

KAMATI YA LESENI

Mwenyekiti wa Kamati ya Leseni ambayo ipo chini ya TFF, Lloyd Nchunga aambao ndio waliokagua viwanja pamoja na vilivyofungiwa, anasema vingi vina matumizi mabaya.

“Tulipoenda tulikagua viwanja na baadhi kutoa maelekezo ya namna ya kufanya, ingawa matumizi mabaya ya viwanja yanachangia kwa kiasi kikubwa kuharibika eneo la kuchezea.

“Viwanja vitaendelea kufungwa pale inapogundulika kuwa havijakidhi vigezo ambavyo husababishwa na matumizi mabaya baada ya ukaguzi,” anasema Nchunga

Anasema awali walikuwa wanatoa taarifa za wao kufanya ukaguzi ambapo wamiliki walikuwa wanajiandaa kufanya marekebisho tofauti na pale wanaposhtukiza.

“Tumebaini kwamba tukiotoa taarifa wanafanya marekebisho kwa kuturidhisha tukiishapita tatizo linarudi palepale, mfano kwenye vyumba ambako tunataka kuwepo na huduma zote zinazohitajika kama mabenchi, ubao wa kufundishia, vyote hivyo viwemo upande wa vyumba vya wachezaji na waamuzi.

“Tuliwapa muda, tunawasubiri wao watupe taarifa kama wamerekebisha, ila awamu hii hatutawapa taarifa ya kwenda maana watajiandaa na tukikuta bado upungufu upo vitaendelea kufungwa ila viwanja vyote vilikaguliwa, hata ule wa Gairo uliokuwa unatumiwa na Mtibwa Sugar nao haufai kutumiwa.” anaeleza Nchunga.

WATAALAMU WA AFYA

Akizungumzia suala la kiafya kwa viwanja vinavyopaswa kutumika, Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa anasema: “Viwanja vikiwa katika hali mbaya wachezaji wengi huumia enka na goti. Kuna viwanja vinadanganya macho. Hivi ni vile ambavyo unaweza ukaviona vina nyasi nzuri kumbe vina mashimo ama vichuguu. Hivyo mchezaji anaweza akajiamini na kutaka kukimbiza mpira au kucheza eneo husika akajikwaa au kuanguka na kusababisha majeraha hasa ya goti au enka.

“Wakati mwingine ni afadhali mchezaji akacheza mahali ambako hakuna majani kabisa kwani atakuwa anajichunga. Athari kubwa ni maumivu ya sehemu za maungio kama vile vifundo, anaweza kuumiza ligamenti au kukatika ‘meniscus’ ambayo inakuwa kama uzi fulani.”