Kocha Tabora United akubali yaishe

KOCHA Mkuu wa Tabora United, Mzambia Simonda Kaunda amesema msimu huu kwao umeisha na hawana cha kupoteza tena, baada ya kikosi hicho juzi kukumbana na kichapo cha fedheha cha mabao 5-0, dhidi ya matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC.
Kichapo hicho kimeifanya timu hiyo kufikisha mechi saba mfululizo za Ligi Kuu Bara bila ya kuibuka na ushindi tangu mara ya mwisho kilipoifunga Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, mechi iliyopigwa Februari 28, 2025.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kaunda alisema morali ya wachezaji wa kikosi hicho imeshuka kwa kiwango kikubwa kutokana na changamoto mbalimbali zilizokuwa nje ya uwezo wao, ingawa jambo la kufurahisha wamejihakikishia nafasi nzuri ya kubaki.
“Kama unavyojua kumekuwa na mambo mengi yanayoendelea yanayochangia hali hii kutokea, ingawa sisi benchi la ufundi kazi yetu ni kuhakikisha tunawajenga kiakili na kimwili, ili tumalize vizuri msimu na tujipange kwa yajayo,” alisema Kaunda.
Kocha huyo alisema kichapo cha mabao 5-0, ilichokipata dhidi ya Azam FC ni kutokana na maandalizi duni waliyoyafanya katika kipindi cha mwezi mzima, ingawa wanajipanga kwa mechi ya kumalizia msimu dhidi ya Coastal Union ya Jumapili Juni 22.
Timu hizo zina kumbukumbu ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1, mara ya mwisho zilipokutana, Desemba 17, 2024.
Simonda alijiunga na timu hiyo, Aprili 18, 2025, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Mzimbabwe Genesis ‘Kaka’ Mangombe, aliyeondoka kutokana na mwenendo mbaya, huku akiiongoza katika mechi nne za kimashindano na kupoteza zote.
Simonda mechi ya kwanza alichapwa mabao 3-0, na Singida Black Stars, Aprili 19, 2025, huku ya pili ni ile ya kichapo pia nyumbani cha bao 1-0 na KMC FC, Mei 14.
Mechi ya tatu ni ya kichapo cha mabao 5-0 kutoka kwa Azam, ambapo kocha huyo aliyewahi kuzifundisha timu za Nkana, Forest Rangers, Chambishi FC na Roan United zote za kwao Zambia, hajashinda tangu ateuliwe.
Kwa sasa timu hiyo imesalia katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa pointi 37, baada ya kucheza mechi 29, ikishinda 10, sare saba na kupoteza 12, ambapo safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho imefunga mabao 27 na kuruhusu 44.