KMC, Yanga kuondoka na Mkenya Prisons?

Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Patrick Odhiambo (kushoto)

WAKATI benchi la ufundi la Tanzania Prisons likilia na mastaa kurudia makosa yale yale hadi kuinyima timu matokeo mazuri, uongozi umetoa mechi mbili kuamua hatima ya Kocha mkuu Patrick Odhiambo.

Prisons imecheza mechi tano mfululizo sawa na dakika 450 bila kuonja ushindi ikiwa ni sare mbili dhidi ya Namungo na Ruvu Shooting, ikipoteza tatu mbele ya Coastal Union mabao 2-0, Geita Gold 4-2 na Kagera Sugar 1-0 na kuporomoka hadi nafasi ya 11 kwa alama 12.

Hadi sasa timu hiyo imecheza mechi 13 ikibakiza miwili kumaliza mzunguko wa kwanza ikiwa ni dhidi ya KMC na Yanga, ambazo watacheza ugenini jijini Dar es Salaam kuamua hatma ya Odhiambo raia wa Kenya.

Msimu uliopita Prisons ilipitia changamoto nzito ya kukwepa kushuka daraja walipoponea kwenye hatua ya mchujo ‘play off’ dhidi ya JKT Tanzania ya Championship kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Shaban Mtupa alisema matokeo si mazuri sana na inawapa wakati mgumu akibainisha wachezaji wanarudia makosa yaleyale kila mchezo na kuwaweka kwenye presha kubwa.

Alisema sehemu ya beki imekuwa na makosa kadhaa ya kuruhusu mabao kila mechi sawa na safu ya ushambuliaji kutotumia vyema nafasi wanazopata na kwamba wanaenda kukaa upya na nyota wao kutathmini mwenendo na kupata mwarobaini.

“Lazima tukiri hali si shwari, matokeo hayafurahishi wachezaji wanafanya makosa yale yale kila mechi, tunapaswa kukaa kuangalia upya jinsi ya kuondokana na hali hii na kujiweka pazuri,” alisema Mtupa.

Katibu Mkuu wa timu hiyo, Anthony Hau alisema matokeo hayawafurahishi akisema mechi mbili zilizobaki kumaliza raundi ya kwanza ndizo zitaamua hatma ya Odhiambo kusalia kikosini au kumpa mkono wa kwa kheri.

“Kwa jumla matokeo yanaumiza sana mechi tatu nyumbani hatuna chochote, lazima tuamke, acha tusubiri mechi mbili hizi za mwisho kumaliza raundi ya kwanza dhidi ya KMC na Yanga,” alisema Hau.

Odhiambo alitua kwa Maafande hao msimu uliopita na kuinusuru timu dakika za mwisho kushuka daraja na mkataba wake unaisha dirisha dogo linaloanza Desemba.