Kipa wa Liverpool kuibebea Zimbabwe

Muktasari:
- Grobbelaar, ana jina kubwa Zimbabwe kutokana na aliyoyafanya kipindi akiichezea Liverpool, aliwahi kuchukua ubingwa wa Kombe la Ulaya ambalo kwa sasa linaitwa Ligi ya Mabingwa.
KIPA wa zamani wa Liverpool, Mzimbabwe, Bruce Gobbelaar ameahidi kutoa msaada wa kiufundi kwenye maandalizi ya Timu ya Taifa ya Zimbabwe ‘The Warriors’ kuelekea Fainali za Mataifa ya Afrika zitakazopigwa Misri.
Grobbelaar alitoa ahadi hiyo akiwa London, wiki iliyopita baada ya kuwasiliana na Kocha wa The Warriors, Sunday Chidzambwa.
Kipa huyo wa zamani wa Zimbabwe, alisema wachezaji wanatakiwa kujengwa kisaikolojia ili morali yao iwe juu kwenye utafutaji wao matokeo kwenye kila mchezo.
“Wachezaji wote wanatakiwa kuwa na kiwango kimoja cha morali, tukifanikiwa hapo mbinu zitakuwa zikituongoza kwenye utafutaji wetu wa matokeo.
“Pia, tutaongea na wachezaji wengine wenye heshima kubwa kwenye taifa letu kama vile Peter Ndlovu, Kaitano Tembo na Benjani Mwaruwaru kwa pamoja tunaweza kuchangia mafanikio ya timu,” alisema.
Grobbelaar, ana jina kubwa Zimbabwe kutokana na aliyoyafanya kipindi akiichezea Liverpool, aliwahi kuchukua ubingwa wa Kombe la Ulaya ambalo kwa sasa linaitwa Ligi ya Mabingwa.
The Warriors itatupa karata yake ya kwanza kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika siku ya ufunguzi dhidi ya wenyeji Misri, Juni 21, itacheza na Uganda, Juni 26 kisha dhidi ya DR Congo, Juni 30.