Kipa wa JKT Tanzania aitaja penalti ya Simba

Muktasari:
- Aliitaja sababu ya kutoisahau mechi hiyo ambayo ni kufungwa dakika za nyongeza bao la penalti na Jean Ahoua wakati dakika 90 za mchezo akiwa ameokoa hatari nyingi akiamini angetoka bila kuruhusu bao.
KIPA wa JKT Tanzania, Yakubu Suleiman amesema tangu msimu uanze mechi iliyosalia katika kumbukumbu zake ni dhidi ya Simba, iliyopigwa Uwanja wa KMC Complex, Desemba 24, 2024.
Aliitaja sababu ya kutoisahau mechi hiyo ambayo ni kufungwa dakika za nyongeza bao la penalti na Jean Ahoua wakati dakika 90 za mchezo akiwa ameokoa hatari nyingi akiamini angetoka bila kuruhusu bao.
“Unapopata cleansheet dhidi ya timu kama Simba, Yanga na Azam FC inaongezea thamani kubwa makipa. Kitendo cha dakika za jioni kufungwa bao la penalti kiliniumiza sana hadi nakumbuka mchezaji wa Simba, Awesu Awesu alinifuata na kunipa moyo kwamba mpira wa miguu ndivyo ulivyo una matokeo ya kikatili,” alisema.
“Lakini msimu kwa ujumla ni mzuri kwa upande wangu katika mechi 28 ambazo JKT Tanzania imecheza nimekosa takribani nane kama siyo tisa, hivyo nimepata nafasi ya kuonyesha kiwango changu.”
Kipa huyo hadi sasa ana cleansheet nane akimtaja Aishi Manula kuwa ndiye aliyekuwa anamvutia wakati anaanza kucheza soka na anaamini ipo siku atafanya vizuri na kuwa kipa tegemeo kwa taifa.
“Mchezaji mwingine ninayemkubali ni kutoka JKT Tanzania anaitwa Salum Gado. Jamaa alikuwa ametoka kozi, hivyo hakuwa tegemeo kikosini ila alifanya mazoezi ya kutosha hadi kuwa panga pangua na akikosekana unaona pengo lake linaonekana, kilichonivutia kwake ni bidii yake,” alisema Suleiman.