Kipa Mbongo Gor Mahia ajipanga

Friday June 19 2020
kisu pic

KIPA David Kissu aliyevunja mkataba wake na Gor Mahia ya Kenya, amesema katika kuhakikisha anakuwa fiti wakati anasubili dili zake zikae sawa aliona bora afanye mazoezi na klabu ya Biashara United inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Awali Kissu alisaini mkataba wa miaka mitatu kuichezea Gor Mahia, lakini mkataba wake umevunjika ndani ya miaka miwili baada ya kutokulipwa mshahara kwa miezi saba.

Akizungumza na Mwanaspoti , Kissu alisema baada ya kurejea nchini alikuwa akifanya mazoezi binafsi na na wenzake wachache lakini Ligi Kuu Tanzania Bara iliporejea, aliona ni vyema ajifue na Biashara United kwa sababu anaishi jirani na maskani ya timu hiyo.

"Ukiwa unafanya mazoezi peke yako ni kweli unaweza usiwe fiti sana lakini mimi kwa upande wangu hivi sasa nafanya mazoezi na Biashara United. Walimu wao wananipa ushirikiano sana kwa kunipa nafasi ya kufanya nao mazoezi," alisema kipa huyo.

Akizungumzia kuhusu mipango yake baada ya kuvunja mkataba na Gor Mahia, alisema uongozi unaomsimamia unapambana kuhakikisha anapata timu nzuri ya kucheza msimu ujao.

"Ofa zipo lakini kama ambavyo unaona hali ya Dunia ilivyo, tuwe na subira kidogo naamini kila kitu kitakuwa sawa tu," alisema Kissu.

Advertisement

Kissu aliibukia katika kikosi cha vijana cha Simba, baadae aliondoka na kwenda Njombe Mji kisha Singida United na ndipo alipopata dili la kwenda Gor Mahia.

Advertisement