Kipa Kagera Sugar aula Burkina Faso

Muktasari:
- Burkina Faso ilimaliza katika nafasi ya nne kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zilizofanyika mwaka huu huko Cameroon.
Licha ya kusotea benchi katika kikosi cha Kagera Sugar, kipa Nourdine Balora amechaguliwa katika kikosi cha Burkina Faso kinachojiandaa na mechi mbili za kimataifa za kirafiki dhidi ya Kosovo na Ubelgiji, Machi 26 na 29 mwaka huu.
Balora ambaye msimu uliopita aliitumikia Namungo, kwa sasa ni chaguo la tatu katika kikosi cha Kagera Sugar nyuma ya Said Kipao na Ramadhan Chalamanda.
Kaimu kocha mkuu wa Burkina Faso, Oscar Barro amemjumuisha Balora katika kundi la makipa watatu kwenye kikosi hicho kilichosheheni nyota wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya.
Kundi kubwa la nyota walioshiriki fainali za Afcon mwaka huu na kuiwezesha Burkina Faso kumaliza katika nafasi ya nne wakiongozwa na nahodha, Bertrand Traore anayeichezea Aston Villa ya England.
Moyo wa ulinzi wa Burkina Faso katika kikosi hicho utakuwa chini ya Edmund Tapsoba wa Bayer Leverkusen ya Ujerumani ambaye alionyesha kiwango bora kwenye fainali za Afcon.
Kocha Barro ameendelea kutoa fursa kwa nyota wachache wanaocheza soka katika klabu za ndani ya Afrika wakiongozwa na beki wa kati na nahodha msaidizi wa RS Berkane, Issofou Dayo.
Baada ya kuonyesha kiwango bora kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Simba, RS Berkane na US Gendarmerie, kiungo wa Asec Mimosas ya Ivory Coast, Stephane Ki naye amejumuishwa katika kikosi hicho cha kocha Barro.
Lakini pia viungo wawili waliopata umaarufu mkubwa katika fainali za Afcon, Adama Guira na Gustavo Sangare wameitwa katika kikosi hicho cha Burkina Faso.
Kikosi kamili kinaundwa na makipa Herve Koffi, Farid Ouedraogo na Nourdine Balora wakati mabeki ni Edmund Tapsoba, Issofou Dayo, Steeve Yago, Issa Kabore, Nasser Djiga, Oula Traore, Soumaila Ouattara na Abdoul Guiebre.
Viungo walioitwa ni Adama Guira, Blati Toure, Gustavo Sangare, Ismahila Ouedraogo, Bryan Dabo, Cedric Badolo, Trova Boni na Stephane Ki.
Kundi la washambuliaji wa kikosi hicho linaundwa na Bertrand Traore, Dango Ouattara, Boureima Bande, Cyrille Bayala, Mamady Bangle, Cheick Ouattara, Fessal Tapsoba, Joffrey Bazie, Noufou Zagre na Abou Ouattara.