Prime
Simba yamnyatia beki wa Al Hilal

KIPIGO ilichopokea Simba kutoka kwa Yanga kwenye Dabi ya Kariakoo, kimewaumiza mashabiki wa timu hiyo ambao wanaamini msimu ujao watarudi wakiwa imara zaidi huku wakitaka maboresho ya kikosi yaendelee kufanyika.
Ombi hilo la mashabiki limesikiwa na viongozi wa Simba ambao wameanza mchakato wa kuboresha kikosi kwa kufanya mazungumzo na beki kushoto wa klabu ya Al Hilal ya Sudan, Khadim Diaw (26), ili kumuongezea nguvu Mohamed Hussein 'Tshabalala'.
Klabu ya Simba ilimuona beki huyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF) ambapo alicheza mechi 12 na alikuwa na kadi za njano mbili.
Endapo dili lake likifanikiwa kuna uwezekano mkubwa wa klabu hiyo, kulikata jina la beki wa kigeni Valentin Nouma raia wa Burkina Faso aliyesajiliwa msimu ulioisha akitokea FC Lupopo ya DR Congo.
Chanzo cha ndani kutoka klabu hiyo kilisema: "Simba ipo katika mchakato wa kuzungumza na wachezaji mbalimbali wazawa na wageni ili kuboresha timu kwa ajili ya msimu ujao."
Chanzo hicho kiliongeza: "Mambo yakienda sawa kuna wachezaji ambao wataachwa, kulingana na ripoti ambayo kocha Faldu Davis ataiandika, kwani msimu ujao Simba ina mipango mikubwa ya kupambania taji la CAF na Ligi Kuu."
Chanzo hicho kilisema kuhusu Tshabalala viongozi wana mpango wa kumuongezea mkataba mpya na mazungumzo baina ya uongozi na mchezaji yamefika pazuri.
"Tshabalala ni mchezaji kiongozi katika timu ndiyo maana tunahitaji kumuongezea nguvu, kwani anatumika sana kuna muda atahitaji mapumziko ama mtu wa kumpa changamoto ya ushindani wa namba," kilisema chanzo hicho.
Maoni ya mshambuliaji wa zamani wa Simba, Steven Mapunda 'Garrincha' alisema kwa ajili ya msimu ujao Simba inahitaji maboresho baadhi ya maeneo: "Upande ambao anacheza Tshabalala na Shomari Kapombe unahitaji kuongezewa watu, mshambuliaji mmoja na beki wa kati."
Simba iliyokuwa uwanjani jioni ya jana kumalizana na Yanga katika kiporo cha Dabi ya Kariakoo msimu ujao itarejea katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya msimu huu kucheza Kombe la Shirikisho na kufika fainali na kupoteza kwa jumla ya mabao 3-1 mbele ya RS Berkane ya Morocco.