Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KIMEO: Arsenal na ugonjwa wao wakufungwa mechi kubwa

Wenger

Muktasari:

Hata hivyo, baadaye mbio zao za kusaka taji la kwanza la ligi hiyo baada ya kulisubiri kwa muda mrefu zilifika ukingoni na wakashuka hadi kwenye nafasi ya nne.

MSIMU uliopita, hakuna timu yoyote iliyoongoza msimamo wa Ligi Kuu England kwa muda mrefu kuliko Arsenal.

Hata hivyo, baadaye mbio zao za kusaka taji la kwanza la ligi hiyo baada ya kulisubiri kwa muda mrefu zilifika ukingoni na wakashuka hadi kwenye nafasi ya nne.

Tatizo lao kubwa linaloisumbua timu hiyo inayonolewa na Profesa Arsene Wenger ni ugonjwa wao sugu wa kushindwa kushinda mbele ya timu kubwa inazoshindania nazo ubingwa.

Vichapo vikubwa vya ugenini kwa Manchester City, Liverpool na Chelsea viliwatibulia, lakini zaidi ilishindwa kupata matokeo mazuri ilipocheza Emirates dhidi ya vigogo hao ikiwamo Manchester United.

Kama Arsenal ingepata pointi nyingi kutoka kwa timu hizo msimu uliopita ingebeba ubingwa.

Tangu mwaka 2009, Arsenal imecheza mechi 30 na timu za ‘Top Four’ na imeshinda mara saba tu, sare tano na kufungwa mara 18. Kwenye vichapo hivyo yamo pia matokeo ya mabao 8-1 waliyokumbana nayo kutoka Man United.

Yachapwa 6-3 na Man City Etihad

Wakati mwaka huu ukiwa safi kwa Arsenal kwenye mechi yake dhidi ya Manchester City baada ya kuwachapa 3-0 Uwanjani Wembley kwenye Ngao ya Jamii, msimu uliopita miamba hiyo ya Etihad ndiyo iliyoanza kutibua sherehe ya Wenger.

Desemba 14, 2013, Wenger na kikosi chake alikwenda Etihad kusaka matokeo mazuri ambayo yangemfanya ajiweke pazuri, lakini tatizo lilelile lilowahi kuelezwa na nahodha wao wa zamani, Cesc Fabregas kwamba Arsenal inaogopa mechi kubwa. Wakachapwa mabao 6-3 na kuwafanya Man City kuibua matumaini ya kubeba ubingwa wa ligi, kitu ambacho walikitimiza mwisho wa msimu.

Yapigwa mabao 5-1 na

Liverpool

Jumamosi ya Februari 8, mwaka huu, Arsenal ilisafiri hadi Anfield kwenda kumenyana na Liverpool.

Liverpool ikiwa kwenye kasi ya kuusaka ubingwa iliishushia kipigo kizito Arsenal baada ya kuwakung’uta magoli 5-1 na kuwapoteza kabisa uwanjani. Ushindi huo mkubwa ulikuwa wa pili kwa Liverpool kuupata dhidi ya Arsenal tangu Aprili 8, 2008, wakati waliposhinda mabao 4-2.

Kwa kipigo hicho cha mwaka huu kocha Wenger alipigwa picha akianguka na mabegi yake kwenye kituo cha treni wakati alipokuwa akitoka Anfield kushuhudia timu yake ikiteketezwa vibaya uwanjani.

Chelsea yaendeleza majanga, yaipiga 6-0

Ni kipindi cha mwezi mmoja tu kutoka kuambulia kipigo kizito Anfield, Arsenal ilikwenda Stamford Bridge ambako pia ilikumbana na majanga mazito.

Samuel Eto’o, Andre Schurrle, Eden Hazard, Oscar alifunga mara mbili na kisha Mohamed Salah kuhitimisha la mwisho katika mchezo uliomshuhudia Jose Mourinho akizidi kumtambia Wenger kwa kumchapa kila wanapokutana.

Mbaya zaidi mechi hiyo ilikuwa ya 1,000 kwa kocha Wenger tangu alipoanza kuinoa Arsenal na kuchapwa mabao 6-0 ilikuwa ni aibu kubwa kwake. Arsenal ilicheza pungufu baada ya mchezaji wao mmoja, Kieran Gibbs kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kosa la lililofanywa na kiungo Alex Oxlade-Chamberlain.

Yashindwa kuifunga Man United goigoi

Timu nyingi sana za kawaida kwa msimu uliopita zilivuna matokeo mazuri kwenye mechi zao walizocheza dhidi ya Man United iliyokuwa chini ya David Moyes, lakini Arsenal ilishindwa kupata ushindi.

Man United ilionekana kuwa timu dhaifu, lakini ilipokwenda Emirates, Arsenal ilishindwa kupata ushindi na kufanya mechi hiyo kumalizika kwa sare ya bila kufungana. Matokeo hayo yalikuwa mabaya kwa Arsenal kwa sababu walicheza mechi hiyo ikiwa ni siku chache tu zimepita tangu ilipotoka kuchapwa na Liverpool.

Kwenye mechi yao ya kwanza waliyocheza Old Trafford, Arsenal iliendeleza ugonjwa wake wa kufungwa mechi kubwa baada ya kuchapwa bao 1-0, Novemba 10, 2013.

Watajiuliza kwa Man City?

Msimu uliopita, straika Lukas Podolski mara kadhaa aliwataka wenzake wakaze buti uwanjani kwa sababu walipoteza mechi zao nyingi kubwa walizocheza muda wa maakuli.

Wakiwa na kumbukumbu ya kupigwa mabao 6-3, Arsenal leo Jumamosi mchana itarudi Uwanjani Emirates kumenyana na Man City kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu. Man City itahitaji kulipa kisasi cha kufungwa kwenye Ngao ya Jamii na Arsenal itahitaji kukwepa aibu iliyowakuta mwaka jana.

Ikiwa na nyota wake wapya kwenye safu ya ushambuliaji akiwamo Alexis Sanchez na Danny Welbeck, Arsenal itaweza kupata matokeo mazuri na kuondoa jinamizi la kupoteza mechi kubwa inapocheza kwenye Ligi Kuu? Tusubiri tuone kama itaweza kufuta rekodi ya kufungwa na vigogo.