Kim abadili watatu Stars kuivaa Algeria

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ta Tanzania ‘Taifa Stars’, Kim Poulsen amefanya mabadiliko ya wachezaji watatu katika kikosi kitakachoanza leo kwenye mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya Algeria kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Katika kikosi hicho kitakachojitupa uwanjani kuanzia saa 1:00 usiku, Kim amebadili wachezaji watatu tu ukilinganisha na wale walioanza katika mchezo dhidi ya Niger Juni 4, mwaka huu na kupata sare ya bao 1-1.
Beki wa kulia, Shomari Kibwana ameingia kuchukua nafasi ya Haji Mnoga, kiungo Mzamiru Yassin amechukua nafasi ya Himid Mao na beki anayeweza kucheza pia kama Winga, Nickson Kibabage amechukua nafasi ya George Mpole.
Wachezaji wengine ni wale wale walioanza dhidi ya Niger ambapo langoni ataanza Aishi Manula huku, Mohamed Hussein, Kibwana, Dickson Job na Bakari Mwamnyeto wakicheza eneo la mabeki.
Viungo wataanza Mzamiru, Novatus Dismas na Feisal Salum na nahodha Mbwana Samatta atatumika kama nshambuliaji wa kati huku Kibabage na Simon Msuva wakicheza kama mawinga.
Benchi wapo Metacha Mnata, Aboutwalib Mshery,Lusajo Mwaikenda, Kennedy Juma, Salum Abubakar, Kibu Denis, Farid Mussa, George Mpole, Ben Starkie, Joshua Ibrahim, Kelvin John na Abdul Suleiman.
Taifa Stars inahitaji ushindi kwenye mchezo huu dhidi ya Algeria ili kuongoza kundi F lenye timu nyingine mbili za Uganda na Niger kwa alama nne na kuendeleza matuamaini ya kufuzu Afcon 2023.