Kilichowang'oa Kagere, Mugalu Simba chatajwa

ZIMEBAKI saa kadhaa kabla ya Simba kufanya tamasha lao la kibabe la Simba Day litakalotumika kutambulisha nyota wapya na jezi mpya za timu hiyo, huku Kocha Zoran Maki akianika kilichomfanya awapige chini nyota watatu wa kigeni aliokuwa nao kambini nchini Misri.

Washambuliaji Meddie Kagere na Chris Mugalu pamoja kiungo mkabaji, Taddeo Lwanga walirejesha Tanzania kutoka kambini jijini Ismailia, licha ya wao kuwa wachezaji 19 wa kwanza katika kambi hiyo iliyovunjwa katikati ya wiki hii na timu hiyo kurejea nchini Alhamisi.

Kagere tayari keshajiunga na Singida Big Stars iliyopanda Ligi Kuu Bara msimu huu, huku Mugalu na Lwanga wakiwa bado haijafahamika wanaelekea wapi baada ya kuagwa rasmi na klabu hiyo ambayo leo Jumatatu watafanya tamasha la Simba Day likiwa ni la 13 tangu liasisiwe 2009.

Hata hivyo kocha Zoran akizungumza na Mwanaspoti aliweka bayana kilichomfanya awateme nyota hao licha ya kuanza nao kambi nchini Misri na kusema kikosi chake kilikuwa na wachezaji wengi wa kigeni kwa maana hiyo alitakiwa kuwapiga panga watatu kwa vigezo vya viwango vyao.

“Kwa kushirikiana na wasaidizi wangu tulikubaliana hao wachezaji ndio wa kuachana nao na nafasi zao kuchukuliwa na wengine tunaamini katika uwezo wao na naamini watapata nafasi ya kwenda kucheza katika timu nyingine, lakini ilikuwa lazima nipunguze kubaki na wanaohitajika,” anasema Zoran na kuongeza; “Wachezaji wapya waliochukua nafasi zao wamenipa uhakika wa kutoa vitu bora kwa maana ya uwezo wa kutimiza majukumu yao kuliko wao.”

Kocha huyo aliyechukua nafasi ya Pablo Franco, alisema Simba ilihitajiwa kuwa na wachezaji 12 wa kigeni wa mashindao hasa ya ndani kwa mujibu wa kanuni inayoruhusu nane kucheza mechi moja na kwa kuzingatia viwango vya msimu uliopita ilikuwa lazima awafyeke kikosini.

Nyota hao kila mmoja alikuwa amesaliwa na mkataba wa mwaka mmoja, hivyo wameshamalizana na mabosi wa klabu hiyo na kuanza maisha mapya na Kagere aliyewahi kuwa Mfungaji Bora wa Ligi kwa misimu miwili mfululizo, msimu uliopita alifunga mabao saba, huku Mugalu akimaliza msimu bila ya bao licha ya msimu mmoja nyuma alifunga mabao 15 akiwa nyuma ya kinara John Bocco aliyetwaa tuzo ya Mfungaji Bora akimpokea Kagere.

Bocco msimu uliopita alifunga mabao matatu tu, kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya kila mara kama ilivyokuwa kwa Mugalu.