Kilichomng’oa Kally Ongala KMC

Muktasari:
- Taarifa kutoka katika timu hiyo, zimeliambia Mwanaspoti kuwa, Kally na viongozi wa kikosi hicho kwa sasa hawaelewani kutokana misuguano ya ndani kwa ndani, jambo linalochangia kufanya vibaya na kujiweka kwenye hatari ya kushuka daraja msimu huu.
UONGOZI wa KMC umevunja mkataba na Kocha Mkuu, Kally Ongala kutokana na mwenendo mbovu wa kikosi hicho msimu huu katika Ligi Kuu tangu alipojiunga nacho Novemba 14, 2024.
Taarifa kutoka katika timu hiyo, zimeliambia Mwanaspoti kuwa, Kally na viongozi wa kikosi hicho kwa sasa hawaelewani kutokana misuguano ya ndani kwa ndani, jambo linalochangia kufanya vibaya na kujiweka kwenye hatari ya kushuka daraja msimu huu.
“Kumekuwa na matabaka kwa wachezaji na kocha ndio maana hata kiwango chetu kimekuwa sio cha kuridhisha, ingawa ukiwa nje unaona timu inacheza vizuri. Makubaliano tuliyofikia ni ya pande mbili ya kusitisha mkataba,” kilisema chanzo.
Mtu wa karibu na kocha huyo alipotafutwa kuzungumza hayo na Mwanaspoti baada ya Kally kudai hayupo sehemu nzuri, alisema baadhi ya viongozi wanamuingilia kazini, jambo ambalo hakuwa tayari kuona.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula alipotafutwa na Mwanaspoti kwa ajili ya kuzungumzia suala hilo, alisema kama viongozi watatoa tamko rasmi, ingawa kwa sasa kinachoendelea ni taarifa za mtandaoni ambazo hawezi kuzielezea.
Hata hivyo akizungumza kupitia kituo kimoja cha televisheni, msemaji wa timu hiyo, Khalid Chukuchuku alithibitisha kuwa wameachana naye.
Kally aliyewahi kuifundisha Azam akiwa kocha wa muda na kocha wa washambuliaji, alijiunga KMC akichukua nafasi ya Abdihamid Moallin aliyejiuzulu Novemba 11, 2024, kisha akajiunga Yanga.
Moallin hadi anajiuzulu katika kikosi hicho alikiongoza kwenye mechi 11 za Ligi Kuu Bara msimu huu, ambapo kati ya hizo kilishinda nne, sare mbili na kupoteza tano akikiacha nafasi ya saba na pointi 14.
Kwa upande wa Kally amekiongoza katika mechi 15 za ligi Kuu kati ya hizo kishinda nne, sare nne na kupoteza saba, ingawa kiujumla KMC imecheza 26, ikishinda nane, sare sita na kupoteza 12 ikiwa nafasi ya 11 na pointi 30.