Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilichomkuta Feitoto Azam FC

Muktasari:

  • Fei Toto ndiye mchezaji aliyefanya vizuri zaidi kwa mwaka 2024, ambapo kiungo huyo alichangia mabao 27 ya Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga 15 na kuasisti 12, akimpiga bao, Stephane Aziz KI wa Yanga aliyefunga 12 na kuasisti tisa.

KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, ameuanza vibaya mwaka huu wa 2025 tofauti na uliopita baada ya kutofunga bao lolote katika Ligi Kuu hadi sasa, licha ya kuasisti mabao manne kati ya asisti zake 13 akiwa kinara.

Fei Toto ndiye mchezaji aliyefanya vizuri zaidi kwa mwaka 2024, ambapo kiungo huyo alichangia mabao 27 ya Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga 15 na kuasisti 12, akimpiga bao, Stephane Aziz KI wa Yanga aliyefunga 12 na kuasisti tisa.

Mwaka 2024, Feisal aliongoza kwa nyota waliochangia mabao mengi akifuatiwa na Stephane Aziz KI aliyechangia 21, baada ya kufunga 12 na kuasisti tisa, huku Gibril Sillah wa Azam FC akihusika na mabao 13, akifunga manane na kuasisti matano.

Kiwango bora cha Fei kilimfanya kumaliza na mabao 19 ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita 2023-24, akiwa ndiye mchezaji mzawa aliyeshika nafasi ya kwanza kwa kufunga mabao mengi zaidi, nyuma ya Aziz KI wa Yanga aliyeibuka kidedea kwa kufunga 21.

Pia, alikuwa mchezaji bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), msimu uliopita baada ya Azam FC kufika fainali na kuchapwa na Yanga kwa penalti 6-5, kufuatia suluhu (0-0) ya dakika 120 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar Juni 2, 2024.

Mbali na hilo, Fei Toto aliiwezesha Azam FC kurejea katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka 10, tangu mara ya mwisho kikosi hicho kiliposhiriki 2015, kufuatia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2013-2014.

Fei Toto hadi sasa kwa msimu huu wa 2024-25 katika Ligi Kuu akiwa na kikosi hicho cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, amehusika katika mabao 17, baada ya kufunga manne na kuasisti mengine pia 13, akiwa ndiye mchezaji anayeongoza kwa asisti nyingi zaidi.

Licha ya kiwango hicho, lakini Fei Toto kwa sasa hajafunga bao lolote la Ligi Kuu kwa mwaka 2025, tangu mara ya mwisho nyota huyo alipofunga ugenini katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 3-1, dhidi ya Dodoma Jiji, mechi iliyopigwa Desemba 1, 2024.

Akimzungumzia Fei ambaye msimu huu anacheza nyuma zaidi tofauti na msimu uliopita ambao alitumika kama straika, kocha wa Azam FC, Rachid Taoussi alisema ni jambo la kawaida kumtokea mchezaji yeyote, ingawa suala la kufunga sio jukumu lake, japo ikitokea nafasi ya kufanya hivyo atafanya kama ambavyo ameonyesha kwa mechi nyingine.

“Napenda kile anachokifanya uwanjani kwa kushirikiana na wenzake, siwezi kusema ni lazima afunge kwa sababu ni miongoni mwa wachezaji ambao kila mmoja wetu anajua uwezo wake, sisi kama benchi letu la ufundi tunajivunia sana yeye,” alisema.

Fei Toto aliyejiunga na kikosi hicho cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Juni 8, 2023 akitokea Yanga, mkataba wake na timu hiyo unaisha mwakani 2026 na inaelezwa huenda asiongeze mwingine ili akatafute changamoto sehemu nyingine.