Kigogo TFF amaliza utata ishu ya Inonga

Muktasari:

  • Inonga aliyesajiliwa na Simba misimu mitatu iliyopita akitokea DC Motema Pembe, kwa sasa hayupo katika kambi ya timu hiyo kwa kilichoelezwa kwamba ametimkia Ufaransa kwenda kujiuguza, huku jana akinukuliwa na Mwanaspoti kwamba huenda ikawa ndio imetoka hiyo kwake kwani mkataba wake upo ukingoni.

SAA chache tangu beki wa kati wa Simba, Henock Inonga kufunguka kwamba mkataba alionao na klabu hiyo unamalizika mwishoni mwa msimu huu, huku mabosi wa Msimbazi wakimkomalia kwamba bado ni mali yao hadi mwakani, lakini kigogo mmoja wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ameamua kumaliza utata wa jambo hilo.

Inonga aliyesajiliwa na Simba misimu mitatu iliyopita akitokea DC Motema Pembe, kwa sasa hayupo katika kambi ya timu hiyo kwa kilichoelezwa kwamba ametimkia Ufaransa kwenda kujiuguza, huku jana akinukuliwa na Mwanaspoti kwamba huenda ikawa ndio imetoka hiyo kwake kwani mkataba wake upo ukingoni.

Hata hivyo, Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alinukuliwa akikanusha msimamo huo wa Inonga akidai bado ni mali yao, kwani bado wana mkataba naye hadi mwakani


Mwanaspoti kwa kutaka kujiridhisha juu ya ukweli uliopo baina ya pande hizo mbili, liliamua kuchimba kutoka ndani ya TFF ambayo mikataba ndio inaposajiliwa na kupenyezew kwamba, Simba wapo sahihi kwa ishu hiyo, kwani Inonga mkataba alionao na Simba utamalizika Juni mwakani na sio msimu huu.

Kigogo huyo aliyekataa kuandikwa jina, ameiambia Mwanaspoti kwamba inawezekana kinachoendelea baina ya pande hizo hawawezi kuingilia, ila ujkweli wanachojua wao (TFF) ni kwamba mkataba wa Inonga na Simba ni hadi mwakani kwani.

"Sipendi kuzungumzia sana hizi ishu za mikataba kwa vile ni suala la klabu na wachezaji, lakini hii inasajiliwa huku na kwa bahati tunachojua ni kwamba huyo beki wa Simba bado ana mkataba na klabu hiyo hadi mwakani," amefichua kigogo huyo wa TFF.

Inonga aliyeutengeneza 'Ukuta wa Yeriko' sambamba na beki Mcameroon, Fondoh Che Malone, alianza kuingia matatani Msimbazi, tangu mechi za Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Novemba 5 mwaka jana ambapo Simba ilipigwa mabao 5-1 kabla ya kulizua upya timu hizo ziliporudiana alipoumia na kumpisha Hussein Kazi ambaye alisababisha penalti iliyozaa bao la kwanza la Yanga kupitia Stephane Aziz KI.

Baadhi ya wana Simba wanaona kama katika mechi hiyo ya Aprili 20 beki huyo alijivunja ili kujitoa lawama kutokana na awali kutajwa kama mmoja ya waliohujumu timu hiyo kiasi cha kudaiwa alikuwa mbioni kusimamishwa na wenzake kadhaa kabla ya mabosi wa klabu hiyo kuahirisha kwa kilichoelezwa uwepo kwa mechi za kimataifa zilizoikabili Simba, japo viongozi wa walilikanusha hilo mapema.

Mara baada ya kipigo cha mechi ya Novemba 5, Simba ilimtimua aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Roberto Oliveira 'Robertinho' na kumleta Abdelhak Benchikha aliyetimka klabuni hapo hivi karibuni.