Prime
Kibu Denis aandaliwa programu maalum Simba SC
Muktasari:
- Davids amefunguka hayo siku chache baada ya kumchezesha mchezaji huyo dakika chache kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya APR timu hiyo ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema kuwa mshambuliaji Kibu Denis bado hajafikia katika ubora anaouhitaji hivyo amemuandalia programu maalum ya mazoezi.
Davids amefunguka hayo siku chache baada ya kumchezesha mchezaji huyo dakika chache kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya APR timu hiyo ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Alisema Kibu ni mchezaji mzuri lakini mwili wake bado haupo tayari kwa mechi za ushindani kutokana na kutokufanya maandalizi pamoja na timu, hivyo anaamini programu aliyompa itamrudisha kwenye mstari.
Kocha huyo alisema anaamini Kibu akiwa katika ubora atakuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Simba hasa kwenye eneo la ushambuliaji ambalo anatamani kuona linatumika vyema kwa wachezaji wake kutumia kila nafasi watakazotengeneza.
"Kulingana na utimamu wa kikosi changu, nimeona nimpe Kibu mazoezi mengine tofauti ili kuwa imara zaidi na tayari kwa asilimia zote kwa sababu nina imani kubwa na mchezaji huyo anaweza akawa chachu ya ushindani kikosini hasa eneo la ushambuliaji," alisema na kuongeza;
"Tunahitaji kuwa na wachezaji walio tayari kiushindani kabla ya kuingia katika michuano ya ligi ya ndani na kimataifa hili nimelifanya kwa asilimia kubwa kwa wachezaji niliokuwa nao Misri kwa upande wa kibu nina kazi ya ziada kutokana na kuchelewa kuungana na timu."
Davids alisema Kibu atakuwa na mazoezi yake maalumu nje ya yale yanayofanywa na wenzake kutokana na kushindwa kuendana na kasi ya waliomtangulia kuanza mazoezi lakini anaamini ataingia haraka kwenye mfumo kutokana na uzoefu wake.
Kibu alikuwa nje ya timu kuanzia mechi za mwisho za msimu uliopita na hakuweza kuungana na kambi ya timu hiyo iliyokuwa nchini Misri kwa wiki tatu.
Nyota huyo ambaye ameongeza mkataba wa miaka kuendelea kuitumikia Simba msimu ulioisha aliifungia timu hiyo bao moja kwenye mechi za Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga timu yake ikikubali kichapo cha mabao 5-1.