Kessy : Kocha Ngorongoro Heroes, ticha Mkwakwani Sekondari

Muktasari:
Katika soka alianza safari ya ukocha mwaka 2008 alipoanza kozi ya awali iliyokuwa ikifundishwa na mkufunzi George Komba na mwaka 2010 alibahatika kuwa miongoni mwa makocha waliokuwa wakipewa kozi ngazi ya kati ‘intermediate’ iliyokuwa ikifundishwa na Salum Madadi, Kibaha mkoani Pwani. Mwaka 2013 alipata nafasi ya kwenda Arusha kuongeza elimu hiyo na kupata leseni C ya Caf iliyokuwa ikifundishwa na Dominic Niyonzima katika Kituo cha Michezo cha Rolling Stone.
MAISHA yanasonga na mambo yanabadilika kutokana unavyoyachukulia kwani kuna msemo usemao “maisha ni kama kioo ukicheka nayo yanacheka, ukinuna nayo yananuna”. Ndivyo maisha yalivyo kwa kila binadamu.
Mapema mwezi huu, timu ya Ngorongoro Heroes ilifanikiwa kubeba ubingwa wa Cecafa U20 michuano iliyofanyika kule Uganda, wakimaliza mashindano hayo kwa mafanikio makubwa bila kupoteza mchezo hata mmoja huku ikiambulia sare ya mabao 2-2 dhidi ya Kenya ambayo ilikubali kichapo cha bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali.
Katika mafanikio ya vijana hao waliokuwa chini ya Kocha Zuberi Katwila pembeni yake alikuwa na msaidizi wake katika harakati za kuhakikisha Tanzania kubeba ndoo na huyo si mwingine, bali Kocha Kessy Juma ambaye leo Mwanaspoti linamtazama kwa undani na maisha yake.
ALIKOANZIA
Kitaaluma ana shahada ya masuala ya biashara (Bachelor of Business Studies) aliyoipata pale Chuo Kikuu cha Kiislamu, Morogoro, kuanzia mwaka 2013 hadi 2016 na pia ana stashahada ya ualimu aliyoipata pale Chuo cha Alharamain kuanzia mwaka 2002 hadi 2004.
Katika soka alianza safari ya ukocha mwaka 2008 alipoanza kozi ya awali iliyokuwa ikifundishwa na mkufunzi George Komba na mwaka 2010 alibahatika kuwa miongoni mwa makocha waliokuwa wakipewa kozi ngazi ya kati ‘intermediate’ iliyokuwa ikifundishwa na Salum Madadi, Kibaha mkoani Pwani. Mwaka 2013 alipata nafasi ya kwenda Arusha kuongeza elimu hiyo na kupata leseni C ya Caf iliyokuwa ikifundishwa na Dominic Niyonzima katika Kituo cha Michezo cha Rolling Stone.
MALENGO
“Siku moja nataka kuwa kocha kutoka Tanzania ninayefundisha soka nje ya nchi kama wanavyofanya makocha wengine wanaokuja hapa nchini, kwa sababu inakuongezea uzoefu na wasifu kwenye kazi,” anasema.
“Siyo kwamba Tanzania hakuna makocha wenye uwezo wa kufundisha nje ya nchi, bali ule uthubutu ndio haupo, nami sitaki kuwa mwoga kwenye hilo, lazima nijaribu na nina imani nitafanikiwa kufika pale ninapohitaji kufika.”
Anasema atafurahi akifanikiwa kufikia lengo hilo analotamani kwa muda mrefu na ndilo linalomuumiza kichwa kwa sasa huku akiamini ipo siku kila kitu kitakuwa freshi na kukaa katika mstari unaopaswa.
“Pamoja na kuwa kocha wa viwango vya juu, lakini nitapambana hadi kuingia kwenye viwango vya kutambulika kama mkufunzi wa Fifa (Fifa Instructor) kutoka Tanzania, hapo nitakuwa nimeitendea haki ndoto yangu,” anasema.
MAFANIKO
Kila kitu kinakuwa na faida pamoja na hasara zake, na kocha huyo amefunguka kuwa licha ya changamoto mbalimbali anazopitia kuna mafanikio mengi nyuma yake na hilo limekuwa faraja kwake hasa anapotazama nyuma alikotoka.
Moja ya mafanikio anayosema, ni kubeba ubingwa wa Cecafa U20 kule Uganda akiwa na Ngorongoro Heroes, na anaona kwamba kuna mlango wa mafaniko kwa upande wake kwenye soka - ndio unazidi kufunguka zaidi ili kufikia malengo ya kuwa kocha wa kimataifa.
Mafanikio mengine ni yale ya kubeba ubingwa wa mkoa mwaka huu akiwa na Eagle Sports Akademy, ushindi wa Mashindano ya Vijana ya Afrika Mashariki na Kati (Ecayfa) mwaka 2013 kule Arusha.
Pia, ubingwa wa mkoa 2016/17 akiwa na Sahare All Stars kisha akaipandisha Ligi Daraja la Pili (SDL) na baadaye Ligi Draja la Kwanza (FDL) msimu huu - ambapo anaendelea kuinoa mpaka hivi sasa.
Moja ya sifa anazoeleza hadi kupata nafasi ya kuwa miongoni mwa benchi la Ngorongoro Heroes kule Uganda ni pamoja na mafanikio aliyoyapata akiwa na Kituo cha Michezo cha Eagle kilichopo Tanga, na Timu ya Sahare All Stars inayoshiriki FDL msimu huu.
Pamoja na hilo, lakini kuwa na uzoefu kwenye soka la vijana kwa muda mrefu eneo ambalo limekuwa na changamoto kubwa kwenye soka la Tanzania, hivyo kwake ni fursa inayoendelea kumpaisha.
Wapinzani wa timu yake kwenye FDL katika Kundi B ni pamoja na Arusha FC, Geita Gold FC, Gipco FC (Geita), Green Warriors, Gwambina FC (Mwanza), Mashujaa FC (Kigoma), Mawenzi FC (Morogoro), Pamba SC (Mwanza), Rhino Rangers FC (Tabora), Stand United FC ya Shinyanga na Transit Camp ya Dar es Salaam.
MWALIMU MKWAKWANI
Nje ya soka, Kessy ni mwalimu wa masomo ya sayansi katika Shule ya Sekondari Mkwakwani mkoani Tanga akibobea zaidi kwenye masomo ya biashara (Book Keeping na Commerce).
Alianza kazi ya ualimu mwaka 2002 katika Shule ya Sekondari ya Alharamain, lakini kutokana na masomo hayo kufutwa kwa muda, akaamua kubadilisha upepo na kuibukia Mkwakwani ambayo ni shule ya serikali kuanzia 2004 mpaka sasa akiendelea kupambana na vijana katika kunoa bongo zao.
RATIBA YAKE
Mwanaspoti lilitaka kujua namna anavyopanga ratiba yake ya soka pamoja na maandalizi ya masomo kwa wanafunzi wake kila kukicha kutokana na anavyopashwa kufanya kama wanavyofanya waajiriwa wengine wa serikali wakiwa shuleni.
“Kwanza nishukuru walimu wenzangu kwa kunisapoti, ratiba zangu haziingiliani hata siku moja kwa sababu soka mara nyingi ratiba yake huwa jioni na shulen, mambo yote nayamaliza kuanzia asubuhi hadi muda unaopaswa kutoka, nakuwa mwaminifu kwenye kutunza muda,” anasema.
“Natumia muda wangu wa ziada kukaa na wanafunzi kila mara kuwafundisha ili kukimbizana na mtalaa wa elimu, hivyo wanafunzi wangu wanafurahia kwa jinsi ninavyokuwa nao karibu na hilo ndilo limenifanya nisione ugumu katika kutimiza majukumu yangu.”
SAHARE FRESHI
Katibu wa Sahare, Jamal Kajia anasema kwao ni faraja kuona timu yao inapata mafanikio, kwani licha ya kocha huyo kuchaguliwa kuifundisha Ngorongoro Heroes, pia wafanikiwa kumtoa mchezaji Kasim Shabani kuwa kwenye timu hiyo ya taifa ya vijana.
“Unapoona kocha anafanikiwa, ujue anachokifanya kwako ni kizuri, tunaushukuru uongozi wa TFF kwa kuona fursa hii ya kocha wetu, kwani tunaamini huko anapata vitu vingine vipya na kuwa faida kwa wachezaji na timu ya Sahare All Stars,” anasema.
KATWIRA NOMA
Hata hivyo, hakuacha kummwagia sifa kocha mkuu wa Ngorongoro Heroes na Timu ya Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila ambaye alikuwa kiongozi wake kwenye msafara wa kuelekea Uganda, akieleza kuwa ni mmoja wa makocha wachache wenye vitu adimu.
“Kwa muda niliokaa na Katwila nimejifunza vitu vingi, kwa haraka huwezi kumjua mtu kama upo naye mbali, lakini najivunia kukutana na kocha huyo hasa kwa muda huu ambao timu yangu ikiwa FDL.”
TUJIKUMBUSHE
Katika mashindano ya Cecafa U20 yaliyoanza Septemba 21 hadi Oktoba 5, matafa 11 yalishiriki baada ya Rwanda kujitoa, huku Kundi C likiundwa na timu tatu za Burundi, Sudan Kusini na Somalia ilhali Kundi A lilikuwa na Uganda, Sudan, Eritrea, Djibouti wakati C lilikuwa na Kenya, Ethiopia, Zanzibar na Tanzania.
Fainali ya michuano hiyo ilizikutanisha Ngorongoro Heroes na Kenya ambapo Wakenya walilala kwa bao 1-0.