Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KenGold ndoto mpya Ligi Kuu

Muktasari:

  • Timu hiyo yenye maskani yake wilayani Chunya mkoani Mbeya, imeshiriki Ligi Kuu msimu mmoja na kushuka daraja na msimu ujao itacheza Championship kujitafuta tena kupanda daraja. Hata hivyo, timu hiyo katika mchezo dhidi ya Coastal Union iliolala 2-1 na kushuka daraja, ilitokea sintofahamu kwa baadhi ya mastaa kusimamishwa kwa kile walichodai kuihujumu timu.

PAMOJA na kukubali kilichoikuta, KenGold imesema itafuatilia njia zilizotumiwa na Mtibwa Sugar na Mbeya City kuhakikisha inarejea tena Ligi Kuu, huku ikitoa msimamo kwa nyota waliosimamishwa kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.

Timu hiyo yenye maskani yake wilayani Chunya mkoani Mbeya, imeshiriki Ligi Kuu msimu mmoja na kushuka daraja na msimu ujao itacheza Championship kujitafuta tena kupanda daraja. Hata hivyo, timu hiyo katika mchezo dhidi ya Coastal Union iliolala 2-1 na kushuka daraja, ilitokea sintofahamu kwa baadhi ya mastaa kusimamishwa kwa kile walichodai kuihujumu timu.

Waliosimamishwa ni kocha wa viungo, Uhuru Selemani, kiungo Sele Bwenzi, straika James Msuva, Steven Duah na Abdallah Masoud ‘Cabaye’ ambao hadi sasa hawapo kikosini.

Katika ligi ya Championship iliyomalizika hivi karibuni, timu za Mtibwa Sugar iliyoshuka msimu uliopita na Mbeya City zimepanda tena Ligi Kuu baada ya kumaliza katika nafasi mbili za juu.

Mkurugenzi wa KenGold, Keneth Mwakyusa ameliambia Mwanaspoti, licha ya matokeo hayo ambayo hawakuyatarajia, wanaenda kujipanga upya ili msimu ujao warudi kwa nguvu.

Mwakyusa alisema watafuatilia mbinu walizotumia Mtibwa Sugar na Mbeya City kurejea haraka Ligi Kuu ili kuwasaidia na wao kurudi mapema, akieleza kuwa kinachohitajika zaidi ni bajeti na maandalizi mazuri.

“Mpira ni pesa, hivyo tutajitahidi kubaki na wale waliofanya vizuri kuendelea nao Championship, lakini ikiwezekana tuongeze nguvu sehemu zinazohitajika ili kufikia malengo, hatukati tamaa,” alisema Mwakyusa.

Mkurugenzi huyo alisisitiza, wachezaji na wengine waliosimamishwa kikosini kwa utovu wa nidhamu, msimamo ni uleule na hakuna atakayerejea kikosini ili kuweka heshima na fundisho kwa wengine.

Alisema haiwezekani watu wanawekeza fedha zao kwenye mpira kusaidia halafu baadhi ya watu wanajiamulia cha kufanya kwa maslahi binafsi akieleza kuwa hataki kuwaona tena.

“Lazima tuachane nao wakatafute maisha kwingine, hii ni kutaka kuweka heshima, nidhamu na fundisho kwa wengine, jambo walilofanya halikuwa zuri japo wanasema tuonyeshe ushahidi bila kujiuliza kwanini watajwe wao,” alisema kigogo huyo.