Ken Gold, Trans ngoma ngumu, Luyuya akila umeme

Muktasari:
- Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa timu hizo kukutana kwenye ligi hiyo iliyoanza jana Septemba 9, ambapo kila upande umeambulia pointi moja
Mbeya. WAKATI Mbeya City jana ikifanya kweli kwa kuanza vyema championship kwa ushindi mnono wa mabao 5-2 dhidi ya Green Warriors, ndugu zao Ken Gold wameshindwa kutamba nyumbani kwa kulazimishwa sare ya 1-1 mbele ya Transit Camp.
Mchezo huo ambao umepigwa leo Septemba 10 kwenye uwanja wa Sokoine jijini hapa ulikuwa wa kwanza katika championship msimu wa 2023/24 abapo kila timu ilihitaji pointi tatu kujiweka pazuri kwenye msimamo.
Transit Camp ndio walitangulia kupata bao dakika ya 56 kupitia kwa Said Luyaya kabla ya wenyeji kusawazisha kwa penalti dakika ya 86 likifungwa na Daud Mshamo baada ya beki wa Maafande hao, Rashid Ally kuushika mpira eneo la hatari.
Hizi ni dondoo za mechi hiyo
Hii inakuwa mechi ya kwanza kwa Ken Gold kupata sare nyumbani dhidi ya wapinzani hao kati ya michezo miwili nyuma kukutana katika uwanja wa Sokoine Mbeya, huku nyingine wakishinda.
Katika mchezo huo Transit Camp imeweka rekodi ya kupata kadi tano za njano ikiwamo moja iliyozalisha nyekundu kwa straika wake Luyuya ambaye alikuwa mkali katika safi ya ushambuliaji na kuifanya timu yake kumaliza dakika 90 kuwa pungufu.
Hii inakuwa sare ya nne katika mechi saba zilizochezwa msimu huu kwenye championship, ikiwa Mbeya Kwanza dhidi ya Polisi Tanzania, TMA na Stand United na Mbuni dhidi ya Biashara United, mechi zilizopigwa jana katika ufunguzi wa michuano hiyo.
Matokeo hayo yanaifanya Transit Camp kukaa nafasi ya sita huku Ken Gold wakiwa chini yao, wote wakiwa na pointi moja kila upande sawa na Mbuni, TMA, Stand United, Polisi Tanzania na Mbeya Kwanza.