Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KELVIN JOHN Kumbe Samatta ndo anampa mzuka

Muktasari:

Baba wa Kelvin ambaye ni fundi ujenzi,   anasema baada ya mwanaye kukua,  alianza kumsapoti kwa kumnunulia viatu vya kuchezea licha ya kutokuwa na uwezo mkubwa kifedha.

NANI anaujua msoto aliopitia nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta? hakuna njia ya mkato hilo analitambua nyota wa Serengeti Boys, Kelvin John ambaye ametokea kwenye familia ya maisha ya chini kama ilivyokuwa kwa Samagoal.
Samatta ambaye kwa sasa anatesa na KRC Genk yake huko Ubelgiji na kuzifanya klabu kadhaa zipigane vikumbo kuwania saini yake,  alikuwa akishindwa kumudu hata gharama za kununua viatu vya kuchezea soka.
Amini usiamini pamoja na udogo wa umri wake Kelvin ni mtoto muhimu kwenye familia yake ambayo inategemea kidogo akipatacho kupitia mchezo wa soka anaocheza.
Mwanaspoti imepata nafasi ya kutembelea kwa kina Kelvin mkoani Morogoro ambako tumezungumza naye kwa kina mshambuliaji huyo akiwa na baba yake.

MZEE AFURAHIA UGENI
Baada ya kutua Morogoro, baba yake na Kelvin aliufurahia ugeni wa Mwanaspoti  na kutania kuwa havutiwi na mwanaye kuitwa Mbappe.
"Napenda likue zaidi jina lake na sio aitwe Mbappe kwa sababu yeye ni  Mtanzania,  huyo anayefananishwa naye ni raia wa huko Ufaransa, " anasema John.

YEYE NA SOKA DAM DAM
Baada ya kutukaribisha na kupiga stori za hapa na pale,  baba wa Kelvin alianza kufunguka namna ambavyo mwanaye alikuwa akipenda soka tangu akiwa na miaka mitatu.
"Alivyoanza kukaa tu,  nilikuwa na tabia ya kumnunulia vitu vya kuchezea kama ilivyo kwa watoto wengine, Kelvin alipendelea zaidi kuchezea mpira.
"Kelvin hajawahi kupoteza mpira ambao nimemnulia, hapo ndipo nilipoona kuwa anaweza kuja kuwa mcheza soka, " anasema.

SAPOTI WANAYOMPA
Baba wa Kelvin ambaye ni fundi ujenzi,   anasema baada ya mwanaye kukua,  alianza kumsapoti kwa kumnunulia viatu vya kuchezea licha ya kutokuwa na uwezo mkubwa kifedha.
"Sijamsapoti kwa kiwango kikubwa sana,  lakini mbali na kumnunua viatu,  nilikuwa nikitoa vijisenti vyangu kwa ajili ya kumkodia baiskeli ili aitumie kwenda nayo mazoezini.
"Siku ambayo nilikuwa nikikosa nilikuwa namweleza awe anatroti maana kutoka nyumbani hadi mazoezini ni umbali mrefu," anasema.

KELVIN NDIO HUYU
Kelvin ambaye anasimamiwa na kituo cha The football house kilichopo Mwanza anavyoonekana ndivyo alivyo,  ni kijana mpole asiyependa kujichangana na makundi mbalimbali ya vijana mitaani.
Baba yake anamwelezea kwa kusema wamemlea mtoto wake kwenye misingi mizuri ya kuwa anasaidia kazi ndogo ndogo za nyumbani,  ikiwemo kuchota maji, kupika na nyinginezo.
"Ukitaka Kelvin aongee matusi,  hapendi kuchokozwa pamoja na kudanganywa, ni rafiki wa kila mtu, " anasema baba huyo wa Kelvin.

MALEZI YAKE UTOTONI
Mama yake alifariki akiwa na umri mdogo kwa hiyo aliwajibika kwenye malezi kwa kiasi kikubwa hapo ndipo niliposota na mwanaye.
"Kuna kipindi alikuwa hali kwa wakati kutokana shughuli zangu za ufundi ujenzi. Nashukuru Mungu kwasababu alinipa mtoto wa kiume kama angekuwa wa kike kwenye mazingira hayo,  ningepata tabu sana, " anasema.

MAISHA SHULENI
John anasema mwenendo wa mwanaye darasani,  ulikuwa mzuri pindi alipokuwa darasa la kwanza hadi la saba lakini mambo yalianza kwenda hovyo Sekondari.
"Naona uwezo wake umepungua Sekondari kwasababu amekuwa akitumika kwenye mashindano mbalimbali,  muda ambao wenzake wanasoma yeye alikuwa akitumika kwenye soka," anasema.
Kwa sasa Kelvin ambaye anategemewa kwenye kikosi cha Serengeti Boys,  yupo kidato cha pili na mwakani ataingia cha tatu  kwenye shule ya Mwanza Center  Open School.

ANACHOWAZA BABA YAKE
Leo au kesho,  anachowaza baba yake na Kelvin ni kuona mwanaye anafanikiwa ili aweze kuikomboa familia ambayo inawatoto wawili na yeye akiwemo pamoja na mdogo wake Christopher mwenye miaka miatatu.
"Nimekuwa nikimwombea sana kwa Mungu  pia huwa namweleza asiwe na jazba,  awe msikivu ili aweze kufikia malengo yake, Kelvin anania na dhamira ya dhati naamini atafika, " anasema.

VYAKULA ANAVYOPENDA
Baba yake na Kelvin,  anasema mwanaye anapenda sana  ugari na mboga za majani huku muda mwingine hupendelea kula sambusa za viazi.
"Ugali ndo chakula chake anachopenda kula mara kwa mara lakini pia Kelvin anapendelea mazima na hunywa maji mengi pindi alapo chakula, " anasema.

UMISSETA ILIVYOMTOA
Baada ya baba yake kumzungumzia Kelvin vya kutosha,  mwanaye huyo naye alianza kufunguka kwa kusema kuwa michuano ya Umisseta imechagia kupiga kwake hatua kwenye soka.
"Nilivyokuwa shule ya msingi,  kuna mwalimu anaitwa Safari Nyerere aliunda timu ya shule,  timu hiyo ndio iliyowakilisha Umisseta kwa shule yetu ambayo ilifanyika mkoani Mwanza.
"Nilifanya vizuri huko na nikachaguliwa kwenye timu ya mkoa,  huko ndipo nilipoonekana na kuchaguliwa kwenye kikosi cha Serengeti Boys," anasema.

MZUNGU AMPIKA KIBABE
Kumbe,  Kelvin  alikuwa kiungo na sio mshambuliaji kama alivyojizolea umaarufu mkubwa nchini  kwa kuwatungua makipa akicheza  kwenye nafasi hiyo.
Kelvin anasema tangu ameanza  kujihusisha na soka alikuwa akicheza nafasi mbili kiungo na winga lakini siku chache baada ya kujiunga na Serengeti Boys,  aliyekuwa mkurugenzi wa ufundi wa kipindi hicho,  Kim  Poulsen alimbadilisha namba.
"Nakumbuka siku yangu ya kwanza kupangwa katika nafasi hiyo nilifanikiwa kufunga mabao matatu 'Hat trick' ulikuwa ni mchezo wa kirafikii dhidi ya Azam B na ndio ukawa mwanzo wangu wa kucheza nafasi hiyo ambayo inanipa umaarufu,"
"Nafurahia zaidi kucheza katika nafasi hiyo na naamini ndiyo itakayonipeleka mbali zaidi katika maisha yangu ya soka, japo hata nikipangwa katika nafasi nilizokuwa nacheza awali naweza kucheza pia si unajua mpira ni akiri ukijua unajua siwezi kusahau," anasema Kelvin.

NYOTA WALIOMVUTIA
Kelvin anasema  anavutiwa  na kiwango cha mshambuliji wa zamani wa Singida United na Tanzania Prisons,  Eliuter Mpepo  ambaye kwa sasa anaichezea Buildcon ya Zambia.
"Napenda uchezaji wake,  Mpepo ananguvu pamoja na kasi,  ningumu kumzuia,  nilikuwa nikijifunza vitu vingi kutoka kwake, " anasema Kelvin.
Kinda hilo la Serengeti Boys,  anasema kwa Ulaya anayevutiwa naye ni mshambuliaji wa Kireno Christiano Ronaldo anayeichezea Juventus ya Italia.

SAFARI  YA MAJARIBIO
Kelvin ambaye amefanya majaribio katika timu mbili anaweka wazi safari, mapokezi na maisha yake katika timu hizo ambazo amebainisha kuwa aliweza kufanya vizuri anachosubiri ni maamuzi ni wapi anaenda.
"Nilianzia katika timu ya HB koge ya nchini Denmark ambako majaribio yangu yalikuwa ni ya wiki tatu wiki ya kwanza ilikuwa ngumu sana kwangu kutokana na hari ya hewa ya nchini huko kuwa ni ya baridi sana nilishindwa kufanya mazoezi kutokana na vidole vyangu kupatwa na ganzi,"
"Mapokezi yao yalikuwa ni mazuri sana kwangu, niliishi nao vizuri kama nipo nyumbani Tanzania baada ya wiki moja kupita nilizoea hari ya hewa na niliendelea na program yangu ya mazoezi kama kawaida mbali na changamoto ya baridi pia nilikumbana na changamoto ya chakula,"
"Kiukweli katika ishu ya chakula iliniwia vigumu sana nilishindwa kula vyakula vya nchini humo wenyeji wangu walilazimika kunitafutia vyakula vya Afrika lakini kutokana na kukaa kwa muda mrefu nililazimika kujifunza kula vyakula vya huko na sasa navimisi,"
Anasema propgramu alizopangiwa katika majaribio yake ilikuwa ni kuanza na vijana wenyeumri wa chini ya miaka 17 kama alivyo yeye alifanikiwa kufanya vizuri, baada ya hapo alipandishwa katika kikosi cha kwanza na alifanikiwa kucheza mchezo mmoja wa kirafiki na alifunga mabao mawili  katika ushindi wa mabao manne walioupata dhidi ya FC Copenhagen.
Kelvin anasema pia alikutana na changamoto ya mfumo ambao ni tofauti na aliouzoea katika timu yake na timu alizowahi kucheza ilimuwia vigumu lakini anamshukuru mungu aliweza kufanikiwa kuendana nao na alifanikiwa kufanya vizuri ndani ya wiki hizo tatu alizokaa nchini humo.
Kwa upande majaribio aliyofanya katika timu ya Ajax Cape Town ya Afrika Kusini anaweka wazi kuwa pia mapokezi yake yalikuwa mazuri na aliona utofauti wa hari ya hewa ya Denmark na nchini huo ambako anabainisha hari ya huko ni sawa na Tanzania.
"Nilifika saa 7 mchana na nilianza program saa 10 jioni sijisifii lakini siku ya kwanza tu nilifanya vizuri kwasababu nilitoa changamoto na nilifanya mazoezi wiki moja tu baada  ya mazoezi ya siku tatu siku ya nne nilicheza mchezo wa kirafiki na Orlando Pirates ya vijana nilifanikiwa kufunga mabao mawili kati ya sita tuliyoshinda,"
"Nimejifunza mambo mengi na nimegundua utofauti wa maisha ya soka ya Tanzania na nchi nilizopita ni tofauti kuanzia mazingira ya michezo hadi maisha ya wachezaji kwa ujumla naamini hiki nilichokipata kitaniongezea mbinu na mazingira mazuri ya kujitambua," anasema.

MALENGO YAKE
"Mimi maisha yangu ni mpira hivyo nategemea kupata mafanikio kupitia soka kikubwa ninachomuomba mungu ni kuniepusha na matatizo yanayotokana na mpira aidha kwa kuvunjika au kusimamishwa kujiusisha na soka kwasababu malengo yangu ni kupambana kucheza soka vizuri ili niweze kucheza Ulaya,"
"Hakuna mchezaji mwenye malengo ya kuendelea kubaki Tanzania  kucheza kila mmoja anatamani kufika mbali zaidi kwa kucheza soka la kulipwa hivyo kutokana na changamoto hiyo ili niweze kufanikiwa kufikia ndoto yangu ni kuhakikisha napambana na kuto kukatishwa tamaa na kuamini ninauwezo na nitaweza kufika ninapopataka," anasema.

SIKU MOJA KABLA YA GEMU
Anasema wakiwa na mchezo wowote siku moja kabla wamekuwa wakikutana timu nzima na kujadiri mbinu za kuweza kuwatoka wapinzani wao na kwa kiasi kikubwa wamekua wakifanikiwa na ndio siri ya wao kupata matokeo mazuri.
"Mbali na kikao cha pamoja na benchi la ufundi sisi kama wachezaji huwa tunakaa pamoja kama ni timu mpya hatujawahi kukutana nayo tunajadiri nammna ya kuwasoma wapinzani na kama ni timu tumeshawahi kucheza nayo tunapangiana majukumu kila mmoja anamkaba mwenzake kwani tunakuwa tunamfahamu mpinzani wetu namna anavyocheza," anasema.

CHANGAMOTO
Anasema hadi hapo alipofika anamshukuru mungu na anajiona ni shujaa sana ni kutokana na kupitia changamoto nyingi tangu malezi yake na hadi katika michakato yake ya kutaka kufanikiwa kupitia soka.
"Nimelelewa na mzazi mmoja tangu nikiwa na umri mdogo mara baada ya Mama  yangu kufariki baba yangu naweza kusema yeye ndiye aliyechangia mimi kufika hapa hakunikatisha tamaa kwa kile nilichokuwa nakiamini alinipa nafasi ya kukifanya,"
"Kuna muda nilikuwa nasahau hadi muda wa kurudi nyumbani kutokana kufanya mazoezi nikiwa nimeunganisha na muda wa kutoka shule, nilikuwa natoka nyumbani kwa miguu hadi uwanjani kwaajili ya mazoezi baba akikosa nauli ya kunipa, muda mwingine namshukuru baba yangu alikuwa akinipa baiskeli,"

TUKIO LA KUHUZUNISHA
"Katika maisha yangu ya soka tangu nimeanza kujihusisha nikiwa na umri mdogo sijawahi kuumia namshukuru mungu na kila siku namuomba aniepushie janga hilo, hivyo tukio langu baya kwangu katika mpira ni kufungwa hasa katika mashindano muhimu,"
"Mfano sito kaa nikasahau siku tulivyofungwa na Uganda katika mashindano ya CECAFA na sisi tulikuwa wenyeji wa mashindano niliumia sana na nilitokwa na machozi kitu hicho hakitakaa kikafutika katika maisha yangu," anasema Kelvin.

TUKIO LA FURAHA
"Tukio langu zuri ni kuisaidia nchi yangu kufanikiwa kutwaa ubingwa COSAFA ambapo mimi ndiye niliyefanikiwa kusawazisha bao baada ya kutanguliwa kwa kufungwa na Angola na baadaye tukawatoa kwa changamoto ya mikwaju ya penati 6-5,"
"Sio mimi nilipiga penati ya mwisho,  niliifanya timu yetu iingie katika changamoto hiyo ya penati ambayo naweza kusema kipa wetu ndio alitubeba baada ya kupangua mpira wa mwisho uliopigwa na wapinzani wetu," anasema

MARA PAAH KATOBOA
Kelvin anasema anatamani kuona baba yake anakaa sehemu nzuri na anaishi maisha ya kifalme kutokana na kipaji chake ambacho mzazi wake amechangia afike hapo alipo sasa hivyo ikitokea amepata fedha nyingi katika usajili wake wa kwanza tu atamjengea baba yake mjengo wa maana.
"Usajili wangu wa kwanza tu kwasababu naamini nitaanzia nje ya nchi basi pesa yangu ya kwanza ni kwaajili ya ujenzi wa nyumba ya baba yangu wala sio kingine baada ya hapo mambo mengine ndio yatafuata,"