Kaze azua lawama Jangwani

Muktasari:

Jumla ya makocha 72 wameomba kurithi nafasi ya Kaze hadi kufikia jana.

Dar es Salaam. Licha ya makocha kuwa sababu wakati mwingine lakini viongozi wa kamati ya usajili ya Yanga wametakiwa kuwajibika ikiwa timu hiyo inafanya vibaya na si kuwabebesha mzigo makocha.

Ndani ya mwaka mmoja, Yanga imewatupia virago makocha watatu, jambo lililowashangaza wadau wengi wa soka, ambao wamewataka wajitathimini kabla mambo hayajaendelea kuwa mabaya kwao.

Tangu Machi mwaka jana hadi sasa timu hiyo ilianza kumuacha Mbelgiji Luc Eymael, ambaye alidumu ndani ya timu kwa mwezi mmoja.

Baada ya kocha huyo akaajiriwa Myugoslavia, Zlatko Krmpotic, ambaye aliweka rekodi ya kukaa muda mfupi ndani ya klabu hiyo kwani alitua Agosti 30 mwaka jana na kutimuliwa Oktoba 3.

Yanga iliendelea kutafuta suluhisho la kikosi chao ili kicheze soka la kueleweka, ambapo Oktoba 20 mwaka jana ilimleta mrundi Cedrick Kaze.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella alisema Kaze alitakiwa kupewa muda kwani jambo la kubadili badili makocha mara kwa mara linaweza kuwapa faida au hasara zaidi.

“Ingekuwa kocha ndiyo alisajili basi alipaswa kuwajibika, lakini kama aliikuta timu, wachezaji wakiwa wameshasajiliwa hakupaswa kufanyiwa hivyo.

“Yanga ilihitaji muda wa kuifanya icheze vizuri zaidi kama wanavyotaka kwa sababu wachezaji wengi ni wapya.Ujue ukibadili badili makocha kila mara inaweza ikawa sawa wakati mwingine ingawa kufanya vizuri kwa muda mfupi inakuwa nadra sana,” alisema.

Beki wa zamani wa Taifa Satars, George Masatu alisema kamati ya usajili ya klabu hiyo ndiyo inatakiwa kuwajibika sababu ndiyo wanasababisha makocha kutimuliwa mara kwa mara kwa muda mfupi.

“Wakati mwingine makocha wanapewa lawama tu kwani unakuta hata hawajahusika na usajili, wanawakuta tu wachezaji lakini timu ikiyumba kidogo wanakuwa wahanga wakati walitakiwa kupewa muda wafanye kazi yao.

“Kamati ya usajili ndiyo wanatakiwa kuwajibika kwa sababu wanailetea hasara klabu mara kwa mara, kila wakati wanavunja mikataba ya makocha na kutakiwa kuwalipa wakati kama wangesajili vizuri yasingetokea haya,” alisema.