Makocha 72 waomba kazi Yanga

Muktasari:

Makocha wamekuwa wakiomba nafasi  za kurithi mikoba ya Cedric Kaze.

AFISA Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema tangu aondolewe  kocha Cedric Kaze na benchi lote la ufundi, wamepokea wasifu takribani 72  kutoka kwa makocha mbalimbali.

Kaze alifutwa kazi na benchi lote la ufundi baada ya kutoka sare 1-1 katika mchezo wao dhidi ya Polisi Tanzania.

Bumbuli amesema wameendelea kuzichakata CV hizo na bado makocha wameendelea kutuma.

“Si unaona ambavyo tulivyo bize yaani huko ndani watu wanaendelea kuchambua CV, tupo makini kuangalia kocha bora aje katika timu yetu”.

Bumbuli amesema katika makocha waliotuma CV hizo wapo ambao awali waliwahi kutuma na wengine wapya.

“Tunachoangalia ni uzoefu wa soka la Afrika na mafanikio, hilo ndio kubwa ambalo kamati ya Utendaji wanaangalia”.

Ameongeza kuwa mchakato huo unaendelea na watakapofika makocha watano basi hao ndio watakaa chini na kamati ya Utendaji na kuchaguliwa mmoja.

“Utapita mchujo wa nguvu mpaka wabaki makocha watano, wakibaki hao sasa ndio umakini unaongezeka zaidi ili apatikane sasa kocha wa kuja kuinoa timu”.