Kaze amrejesha Carlinhos

Dar es Salaam. Ukimya wa kiungo Carlos Stenio Fernandes Guimaraes do Carmo ‘Carlinhos’ uwanjani umemuibua kocha Cedric Kaze.
Carlinhos miongoni mwa nyota wa Yanga waliopokelewa kwa bashasha wakati akijiunga na timu hiyo Agosti mwaka jana, hajawa na msimu mzuri ndani ya klabu hiyo.
Kocha Kaze alisema alipomuona mchezaji huyo, aliona hafiti kucheza namba 10.
“Carlinhos alikuwa mzuri zaidi akitokea pembeni, bahati mbaya alipata majeraha na sasa anaendelea vizuri na ameanza mazoezi tayari,” alisema.
Kaze alibainisha kwamba mashabiki wajiandae kumshuhudia Carlinhos kwenye mechi ijayo ya Kombe la Shirikisho (FA).
Yanga imetinga hatua ya 16 bora na inasubiri droo ya nani atacheza na nani kwenye hatua hiyo.
“Carlinhos ni mchezaji mwenye mbinu sana, anaelewa na anajua, lakini ni mzuri zaidi akitokea pembeni, naamini atafanya kile ambacho mashabiki wanakitarajia kutoka kwake na habari njema kwao ni kwamba amepona na anaendelea vema na mazoezi.
“Nilifanya usajili wa Fiston (Abdul Razak) ili kupata mtu sahihi ambaye ataitendea haki namba 10, mwanzo alijaribu kucheza Carlinhos, Niyonzima (Haruna), Kaseke (Deus) na Farid (Mussa) wote hawakufiti, kwenye nafasi hiyo,” alisema.
“Nilitaka mtu mwenye ‘consistency’ walikuepo sawa walicheza, lakini nilitaka ambaye atatupa matokeo mazuri kila siku katika nafasi hiyo, ndiyo sababu wachezaji wanne tofauti walicheza lakini bado kulikuwa na shida.
Kocha Kaze pia alizungumzia usajili wa Dickson Job, ambaye ni miongoni mwa wachezaji watatu aliowasajili tangu alipotua Yanga.
“Job ni mpango wetu wa muda mrefu, ni mchezaji mzuri ambaye amepitia timu ya taifa katika ngazi zote, ana kipaji,” alisema kocha huyo.