Nchimbi wa Yanga bado anasoma ramani

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Ditram Nchimbi amesema anazidi kujifunza mengi kutoka kwa wachezaji wa zamani hasa, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ aliyekuwa akitamba enzi anasakata kabumbu.
Hivi karibuni Mmachinga aliliambia Mwanaspoti kuwa, anamuona Nchimbi ni mchezaji mzawa anayeweza kuja kuvunja rekodi yake ya mabao katika Ligi Kuu Bara kwa upande wa wachezaji wazawa endapo atatuliza akili yake na kuwa makini kauli iliyompa faraja kubwa straika huyo.
Nchimbi alisema, kwa sasa anatumia vyema ushauri anaoupata kutoka kwa makocha, wachezaji na hata watu binafsi ambao wanamtakia mema katika maisha yake ya soka ili aweze kufikia malengo yake.
“Kwanza nilifurahi sana kuona mtu kama Mmachinga ananiona mimi kwa jicho la tatu na kuona nafaa kuwa kama yeye, nayafanyia kazi mawazo yake na ushauri wake na naonana nae na kuzidi kupata vitu vingi kutoka kwake,” alisema.
Aidha Nchimbi alisema, mpira ndio kazi yake, hivyo wanavyoona watu kama Mmachinga wanamshauri mambo makubwa anajiona ni kama mwenye deni kwao kuhakikisha anafanya kile ambacho wanamtaka akifanye.
Kuhusu michuano ya Chan Nchimbi alisema, ni moja ya ndoto zilizokuwa katika maisha yake, na anamshukuru Mungu kwa kuzifikia kwani bado anaamini kuna makubwa zaidi huko mbeleni.
“Kupata nafasi katika timu ya Taifa ni moja ya ndoto zangu hivyo huwa natamani kufanya makubwa zaidi ili kuisaidia timu yangu ya taifa kufika mbali,” alisema Nchimbi.