Kariakoo Derby yasogezwa mbele

Wednesday October 07 2020
derby pic

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imesogeza mbele mechi ya Yanga dhidi ya Simba 'Kariakoo Derby' iliyokuwa imepangwa kuchezwa Oktoba 18 na sasa itachezwa Novemba 7 katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa leo Oktoba 7, 2020 imesema kuwa mabadiliko hayo yanatokana na vikazo vya usafiri vinavyoweza kujitokeza baada ya mechi za kirafiki za kimataifa za kalenda ya Fifa ambazo wachezaji wa klabu hizo mbili watashiriki kwenye mataifa yao

“Mabadiliko hayo yametokana na uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa vikwazo katika usafiri wa kimataifa baada ya kukamilika kwa michezo ya kimataifa iliyo kwenye kalenda ya FIFA jambo ambalo linaweza kuathiri vikosi vya klabu hizo mbili” imesema sehemu ya taarifa ya TPLB.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa nchi nyingi bado zimeendelea kuweka masharti magumu katika safari kutokana na janga la covid-19

“Nchi nyingi bado zimeendelea kuweka masharti magumu katika taratibu za usafiri wa kimataifa tangu kuzuka kwa janga la virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa covid-19” imesema taarifa hiyo.

Kuahirishwa kwa mechi hiyo ni muendelezo wa mabadiliko ya ratiba ambayo yamekuwa yakifanywa na Bodi ya Ligi ambapo hivi karibuni iliamua kuahirisha mechi za raundi ya sita ya Ligi Kuu ili kupisha ratiba ya mechi za kimataifa.

Hata hivyo mchezo huo wa Novemba 7 unaweza kuahirishwa tena kwani Novemba 9 kutakuwa na mchezo baina ya timu ya Taifa 'Taifa Stars' na Tunisia utakaochezwa huko Tunis, Tunisia wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon)

Advertisement
Advertisement