Kapombe aanika ramani ya robo fainali CAF

KIKOSI cha Simba kinajiandaa kushuka uwanjani usiku huu kumalizana na TRA ya Kilimanjaro katika mechi ya kiporo cha 32 Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kabla ya kuigeukia Jwaneng Galaxy kwa ajili ya pambano la Kundi B la kufungia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wakati hali ikiwa hivyo, beki wa timu hiyo, Shomari Kapombe ameanika ramani nzima ya timu hiyo kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa bele ya Wabotswana hao.
Simba itavaana na Jwaneng, Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na matokeo ya ushindi yataivusha hadi robo fainali ya michuano hiyo, kwani kwa sasa ina pointi sita ikishika nafasi ya pili nyuma ya Asec Mimosas iliyofuzu mapema ikiwa na pointi 11.
Kutokana na kutambua ugumu na umuhimu wa mchezo huo, beki wa timu hiyo, Kapombe, amesema nidhamu na kujituma mbele ya Jwaneng ndio silaha itakayowabeba Jumamosi, kwani ni lazima washinde ili waende robo fainali.
Hii ni mara ya nne kwa timu hizo kukutana kwenye michuano ya CAF, awali zilishakutana kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2021-2022 na Simba kutolewa kwa kanuni ya bao la ugenini licha ya matokeo ya jumla kuwa sare ya mabao 3-3, Mnyama ikishinda ugenini 2-0 kisha kufungwa 3-1 Kwa Mkapa na mechi ya msimu huu iliyopigwa jijini Francistown, Botswana zilishindwa kutambiana kwa kutoka suluhu.
Akizungumza na Mwanaspoti, nahodha huyo msaidizi wa Simba amesema katika mechi ya wikiendi hii wanajua hawatakiwi kabisa kufanya makosa ya aina yoyote na wanapaswa kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu.
Amesemaa katika mechi hiyo wanapaswa kucheza kama timu kutafuta matokeo na cha muhimu kwenye huo mchezo ni Simba kutangulia kupata bao.
"Nidhamu mbovu ndiyo iliyotuponza katika mechi ya misimu miwili iliyopita, kwani tuliridhika na ushindi wa ugenini na wapinzani wetu wakaja na presha ya juu na kusawazisha na mwisho kutufunga na kutung'oa michuanoni, jambo ambalo hatutaki litokee tena msimu huu," amesema Kapombe aliyewahi kuwika akiwa na Azam FC.
Pia beki huyo anayesifika kwa kupandisha mashambulizi na kuasisti, amezungumzia washambuliaji wapya waliosajiliwa kikosini akisema sio kwamba ni wabaya, lakini wanahitaji muda kuweza kuzoea mazingira na bahati mbaya kwao ni kwamba wamejikuta wakiutafuta muunganiko wakati wa mashindano.
"Lakini naamini tutapata muunganiko bora na katika mechi hii na matokeo mazuri yatakuja tu, kwani mazoezini naona kiwango kizuri cha wachezaji wapya ndio maana kocha anawapanga," amefafanua Kapombe, akirejea matokeo ya mechi tano zilizopita za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi kushinda mechi moja kwa idadi kubwa ya mabao ikiifunga Wydad CA ya Morocco kwa mabao 2-0.
Simba imefunga mabao matatu na kufungwa mawili hadi sasa kwenye michuano hiyo ikishinda mechi moja na sare tatu, huku ikipoteza kwa bao 1-0 mbele ya Wydad ambayo nayo itakuwa uwanjani Jumamosi kumalizana na Asec Mimosas mjini Casablanca.