Kanu, Eto'o kukipiga Bongo
NYOTA wa zamani wa Arsenal, Nwankwo Kanu akiambatana na malijendi wengine wakubwa kama vile Samuel Eto'o, Emmanuel Adebayor, Emmanuel Eboue watatua nchini kwa ajili ya mchezo wa hisani dhidi ya wachezaji wa zamani wa Tanzania Septemba 2, 2023 ili kuchangia watoto wenye matatizo ya moyo.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa mchezo huo wa hisani kuchezwa ukanda wa Afrika Mashariki ukiwa chini ya Taasisi ya Kanu ambaye alikumbwa na tatizo la moyo wakati wa uchezaji wake wa soka la kulipwa.
Akizungumzia tukio hilo, mwakilishi wa taasisi ya Kanu, Victor Akpojo alisema, "Tunafuraha kufanya kwa ajili ya jamii, ningependa jambo hili tulipokee kwa sababu ni kwa ajili ya kusaidia vijana wadogo."
Kwa upande wake, mwenyekiti wa Umoja wa Maveterani wa soka la Tanzania,Paul Ambrose alisema,"Sisi kama wachezaji wa zamani tumevutiwa na hili na tupo tayari kushirikiana na wenzetu kwa ajili ya kusaidia jamii, wachezaji wengi wa zamani wamethibitisha kushiriki."
Taasisi ya Kanu ilianzishwa ili kusaidia watoto na vijana wa Kiafrika wasiojiweza, wanaoishi na magonjwa mbalimbali ya moyo nchini Nigeria na nchi nyingine za Afrika, kupata upasuaji wa moyo.
Safari hii ilianzia Uingereza ambapo walengwa wawili wa kwanza wa Foundation, Mwalimu Oluwatofunmi Okude na Miss Enitan Adesola, walifanyiwa upasuaji, katika Hospitali ya Crown London mwaka 2000.
Kile ambacho kitapatikana kwenye mchezo huo wa hisani kitapelekwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambayo kwa Tanzania imekuwa kinara katika matatibabu ya watu wenye matatizo ya moyo.