Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kama Msuva,Twite benchi, mnatokaje?

Kocha wa Yanga, Hans Van Pluijm

Muktasari:

Mzungu Hans Pluijm amefumua kikosi chake kama mara tatu hivi halafu akashika kiuno na miwani akavua kabisa akafuta kwanza jasho machoni ili aone vizuri.

SIKIA hii kwanza. Golini msimamishe Dida, kulia mweke Twite, kushoto Oscar Joshua, katikati waweke Rajab Zahir na Cannavaro, mido pale wasimamishe Said Makapu na Salum Telela. Pembeni sasa huku Msuva kule Coutinho, kati pale mbele mpange Busungu na Matheo Simon.

Hao peke yao unaweza kumkabidhi Patrick Liewig pale Stand United na akachukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara, lakini sasa hicho siyo kikosi cha kwanza cha Yanga, tulia.

Mzungu Hans Pluijm amefumua kikosi chake kama mara tatu hivi halafu akashika kiuno na miwani akavua kabisa akafuta kwanza jasho machoni ili aone vizuri.

Akapiga hesabu zake weee...Unajua alichomalizia kusema. Kama akichemka tena safari hii kuna mkono wa mtu na hakuna jinsi yoyote mtu atatoka salama mbele yao na ametangaza rasmi kwamba amefunga hesabu za usajili liwalo na liwe.

Unajua kinachompa kiburi ni nini? Amepanga vikosi viwili na chenji ikabaki na kila akiangalia Simba na Azam na timu zingine mzuka unampanda sana. Kwa mujibu wa mazoezi ya Yanga baada ya kukamilika kwa usajili, mziki mpya siyo huo niliokutajia hapo juu, asilimia 90 unaweza kuwa kama ifuatavyo; Golini ataanza Barthez, kisha Juma Abdul, Mwinyi, Yondani, Vincent Bossou, Thabani Kamusoko, Mwashiuya, Niyonzima, Ngoma, Tambwe na Kaseke.

Iko hivi; Pluijm ametamka kwamba anaridhishwa na usajili uliofanyika huku akitaja usajili wa Bossou kuwa ni madhubuti kwa kuwapa changamoto wakongwe Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani ambao walikuwa wamejihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza.

“Ujio wa nyota hawa watatu umefunga usajili wangu, nina imani kuwa nimepata kikosi kipana sasa japo nyota hawa wana kazi ya kuhakikisha wanathibitisha hilo uwanjani,” alisema Pluijm.

“Ujio wa huyu beki wa kati (Bossou) ni maalumu kwa kuwapa changamoto Cannavaro na Yondani, kunapokuwa na ushindani ni dhahiri kuwa viwango vinaimarika zaidi, hawatakiwi kujiona kama wamepoteza nafasi zao bali watoe ushindani ili kupata namba.

“Pato Ngonyani na Rajab Zahir nao wana nafasi bado, licha ya kwamba ni chipukizi wanatakiwa kupambana kuthibitisha ubora wao,” aliongeza Pluijm.

Kuingia kwa mastaa hao watatu ni wazi sasa kikosi hicho kitakuwa na vita mpya ya nafasi katika kutengeneza kikosi cha kwanza na vita kubwa itakuwa katika idara tatu muhimu ukiacha ile ya makipa ambayo Ally Mustapha ‘Barthez’ na Deogratias Munishi ‘Dida’ wanaendelea kuchuana vikali.

Pluijm amesema usajili wa nyota watatu uliofanywa na timu yake hivi karibuni umefunga rasmi zoezi hilo. Yanga imekamilisha usajili wa straika Matheo Saimon kutoka KMKM ya Zanzibar, beki Vincent Bossou kutoka Togo na kiungo Thabani Kamusoko kutoka FC Platinum ya Zimbabwe ambao Pluijm ameuita kama usajili wa mwisho.

Usajili huo unaifanya Yanga kufikisha idadi nyota 10 wapya klabuni hapo ukiachana na beki Mghana Joseph Zuttah ambaye alisajiliwa na kisha kutemwa wiki chache baadaye. Timu hiyo ilifanya pia biashara ya straika, Kpah Sherman kwenda klabu ya Mpumalanga Black Aces ya Afrika Kusini.

ULINZI

Safu ya ulinzi ya Yanga inatakiwa kusukwa upya kufuatia kuyumba kwa Cannavaro na Yondani ambao walionyesha wasiwasi katika mashindano ya Kombe la Kagame. Bossou anaweza kuingia katikati yao ili kuimarisha nafasi hiyo ya beki wa kati ukiacha lile badiliko la awali la kuingia Mwinyi Haji aliyemwondoa Oscar Joshua katika beki ya kushoto.

Mtihani wa nani aondoke kati ya Cannavaro na Yondani utateguliwa katika maandalizi hayo ya kambi ya Tukuyu ingawa kazi kubwa atakuwa nayo Cannavaro kutokana na kuwa na aina moja ya uchezaji na Bossou.

Hata hivyo, Pluijm hawezi kukubali timu hiyo iachane na beki yeyote kati ya hao wawili kutokana na ugumu wa ligi na majukumu ya mashindano ya kimataifa mwakani.

KIUNGO

Katika kiungo, mfalme Haruna Niyonzima naye atakuwa na changamoto kubwa itakayomlazimu sasa kufanya kazi ya ziada kupigania nafasi. Changamoto hiyo imeletwa na ujio wa Kamusoko ambaye ameonyesha hana wasiwasi katika kujua kuichezesha timu na kupiga pasi mtambuka kwa washambuliaji wa kati.

Hata hivyo, changamoto hiyo inaweza isiwepo endapo Pluijm ataamua kumchezesha Kamusoko nafasi ya kiungo mkabaji, ambayo alikuwa akiicheza FC Platinum ingawa kiungo huyo ameliambia Mwanaspoti kwamba licha ya kumudu kucheza nafasi ya kiungo mkabaji ambayo sasa inazibwa na mkongwe Mbuyu Twite anapenda kucheza kama kiungo mchezeshaji. Uwepo wa Salum Telela pia umeongeza ushindani katika nafasi hiyo.

USHAMBULIAJI

Yanga wamemsajili Matheo na sasa usajili huo utaongeza vita ya nafasi na kusumbua vichwa cha Pluijm na msaidizi wake Charles Mkwasa kujua nani aanze katika eneo hilo.

Washambuliaji Donald Ngoma na Amiss Tambwe wana nafasi kubwa ya kuanza endapo kombinesheni yao itafanikiwa kufanya kazi vizuri. Endapo watashindwa kufanya hivyo uwepo wa Malimi Busungu na Matheo unaweza ukamwondoa mmoja kati ya hao.

Busungu pia anaonekana kuwa na nafasi kubwa kutokana na uimara wake wa kuzifumania nyavu.