Kaizer Chiefs yamtaka Nabi

Muktasari:
- Vyanzo vya habari kutoka Afrika Kusini na Tanzania vimesema kwamba Nabi anafikiriwa kuajiriwa na timu hiyo kutokana na kiwango cha juu ambacho ameonyesha msimu huu.
TIMU ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini inadaiwa kufanya uchunguzi kuhusu uwezekano wa kufanya mazungumzo na kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi ili akaifundishe.
Vyanzo vya habari kutoka Afrika Kusini na Tanzania vimesema kwamba Nabi anafikiriwa kuajiriwa na timu hiyo kutokana na kiwango cha juu ambacho ameonyesha msimu huu.
Hata hivyo, bado miamba hiyo ya Afrika Kusini wameendelea kunolewa na kocha wao Arthur Zwane, ingawa uongozi wa timu hiyo unataka kufanya mabadiliko ya haraka kabla ya msimu mpya kuanza.
Chiefs walimaliza katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi ya Sauzi wakiwa na pointi 44 ni tofauti ya pointi 26 na mabingwa wa Ligi Kuu Mamelodi Sundowns.
Miamba hao wa Soweto hawajafanikiwa kutwaa taji Ligi Kuu tangu Mei 2015 na wamekuwa na makocha sita tofauti kwa kipindi cha hivi karibuni.
Hata hivyo, Rais wa Yanga Injinia Hersi Said amesema Kocha Nabi ataendelea kubaki klabuni hapo.
"Kila mkataba una kikomo ni kweli mkataba wa Nabi unafikia tamati mwisho wa msimu huu na klabu ilishaanza hatua ya kumuongezea mkataba mwingine," amesema Hersi.