Kaeni kwa kutulia...Bado nane tu!

NAHODHA wa Simba, John Bocco amerejea mchezoni lakini na Simba imebakiza pengo la pointi nane tu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kuikuta Yanga inayocheza na Dodoma Jiji wikiendi hii Jijini Dodoma.

Awali Simba ambao ni mabingwa watetezi walikuwa na gepu kubwa la pointi dhidi yao na vinara Yanga wenye pointi 57 lakini suluhu tatu za vijana hao wa Jangwani zimewapa faida Simba ambao wanaonekana kufukuza mwizi kimyakimya. Simba sasa inafikisha pointi 49, huku wakiwa wamecheza michezo sawa na Yanga 23.

Katika mechi ya jana usiku, gumzo ilikuwa Bocco aliyeonyesha kurudi kwenye makali yake ya kupachika mabao baada ya kufunga bao lake la pili msimu huu kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Kagera Sugar na kushinda mabao 2-0. Huo umekuwa muendelezo mzuri kwa Bocco ambaye hakuwa na mwanzo mzuri kwenye ligi lakini alianza kufunga rasmi Mei 8 mwaka huu kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting akitupia bao la tatu kwenye ushindi wa 4-1.

Matokeo hayo ni kama kisasi cha Simba kwa Kagera kwani mchezo wa duru la kwanza kwenye Uwanja wa Kaitaba Januari 26 Simba ilifungwa bao 1-0, lililopachikwa na Hamis Kiiza ‘Diego’.

Simba ilianza mchezo kwa umiliki wa mpira huku ikitengeneza nafasi za mabao lakini haikuzitumia ndani ya dakika tano za mwanzo ambapo Kagera walipata nafasi moja kupitia kwa Kiiza lakini alipiga mpira na kupaa juu.

Dakika ya 13 Kibu Denis aliifungia Simba bao la kuongoza kwa kumalizia pasi ya Rally Bwalya aliyoipiga akiwa ndani ya boksi la Kagera akiunganisha baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Bao hilo limekuwa la sita kwa Kibu ambaye amekuwa na muendelezo mzuri tangu atue Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Mbeya City.

Baada ya bao hilo, Kagera ilitaka kusawazisha na kupanda kushambulia na Simba kufanya shambulizi la haraka lakini Mzamiru Yassin akiwa na kipa akashindwa kutumia vyema nafasi iliyotengenezwa na Kibu.

Dakika ya 26 beki wa Kagera Sugar, Abdallah Mfuko alipata majeraha na kutolewa nje kwa machela na nafasi yake kuchukuliwa na Stephen Duah.

Simba iliendelea kuishambulia Kagera kupitia upande wa kulia alipokuwa akicheza Kibu na Shomary Kapombe lakini mabeki wa Kagera wakiongozwa na David Luhende walikuwa imara kudhibiti mashambulizi yale hadi dakika ya 35.

Bocco dakika ya 29 aliifungia Simba bao la pili likiwa ni bao lake la pili pia kwa msimu huu kwa kupiga shuti la wastani lililompita kipa wa Kagera Said Kipao na kutinga nyavuni.

Hiyo imekuwa Asisti ya pili kwa Bwalya kwenye mechi ya jana baada ya kufanya hivyo katika bao la kwanza lililofungwa na Kibu.

Licha ya Kagera kujilinda na kushambulia kwa kushitukiza lakini Simba ndiyo ilimiliki mpira kwa kiasi kikubwa na kutengeneza nafasi nyingi za mabao ambazo washambuliaji wake hususani Kibu na Bocco walizipoteza na kutumia mbili tu ndani ya dakika 45 za kwanza.

Katika dakika hizo 45 za kwanza Bocco pamoja na kufunga bao moja, lakini alitumbukiza mara mbili mpira nyavuni na mwamuzi wa kati Ramadhan Kayoko na mwamuzi msaidizi Frank Komba waliamua kuwa alikuwa kwenye maeneo ya kuotea.

Baada ya dakika 45 kumalizika wakati timu zikielekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, kocha wa Simba, Pablo Franco alionyeshwa kadi ya njano kwa kuwalalamikia waamuzi.

Kipindi cha pili kilirejea kwa kila timu kutafuta bao lakini Simba iliendelea kutawala mchezo na dakika ya 50 ilitengeneza nafasi ya bao lakini Kibu akiwa na kipa alishindwa kufunga na kipa wa Kagera Kipao kupangua mpira.

Dakika ya 53 Ally Idd wa Kagera alioneshwa kadi ya njano baada ya kumchezea madhambi Henock Inonga wa Simba na muda huo huo Iddi na Kiiza walitolewa na nafasi zao kuchukuliwa na Mbaraka Yusuf na Erick Mwijage waliingia kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji.

Kagera ilifanya mabadiliko mengine dakika ya 66 kwa kumtoa Hassan Mwaterema na kuingia Meshack Abraham na dakika moja baadae Simba ikawatoa wafungaji wa mabao yake mawili, Kibu na Bocco na kuingia Peter Banda na Meddie Kagere.

Matokeo hayo yameifanya Simba kufikisha pointi 49 ikiendelea kupunguza pengo la alama dhidi ya mpinzani wake Yanga, inayoongoza ligi kwa tofauti ya pointi nane ikiwa kileleni na pointi 57 huku timu zote hizo zikiwa zimecheza mechi 23.

Kagera Sugar imesalia katika nafasi ya saba na pointi 29 na mchezo ujao itacheza na ugenini na Tanzania Prisons huku Simba ikiisubiri Pamba FC ya Championship kucheza mechi ya robo fainali kombe la Azam (ASFC) Jumamosi ya Mei 14.

Katika kipindi cha pili timu hizo zilishambuliana kwa kasi huku Simba ikiendelea kutawala katikati na kupata matokeo mazuri mpaka wanamaliza mchezo huo. Kocha wa Kagera, Mkenya Francis Baraza alisema Simba waliwazidi ujanja baada ya kuamua mchezo mapema na kurudi kujilinda kiakili. Pablo Franco wa Simba alisema; “licha ya ratiba ngumu kwenye michuano hii lakini nashurukuru tumepata pointi, tumetengeneza nafasi nzuri na tumeudhibiti mchezo. Ni matokeo muhimu sana kwetu kwenye mbio hizo.”

Vikosi; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Pascal Wawa, Joash Onyango, Henock Inonga, Pape Sakho, Mzamiru Yassin, John Bocco na Rally Bwalya

Kagera Sugar; Said Kipao, Dickson Mhilu, David Luhende, Nassoro Kapama, Abdallah Mfuko, Appolinaire Ngueko, Hamis Kiiza, Abdallah Seseme, Hassan Mwaterema, Ally Ramadhani na Ally Nassoro.