Jumamosi yaibeba Yanga Kariakoo Dabi

Muktasari:

  • Kitendawili cha nani mbabe kitateguliwa Jumamosi hii ingawa Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa na morali kubwa hasa baada ya mechi yao ya mwisho iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Novemba 5, 2023 kuifunga Simba kwa mabao 5-1.

MASHABIKI wa Yanga na Simba tayari viroho vimeanza kuwadunda, wakati wakiendelea kuhesabu siku kabla ya timu zao kushuka katika pambano la Ligi Kuu Bara litakalopigwa Jumamosi hii ya Aprili 20, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Kitendawili cha nani mbabe kitateguliwa Jumamosi hii ingawa Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa na morali kubwa hasa baada ya mechi yao ya mwisho iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Novemba 5, 2023 kuifunga Simba kwa mabao 5-1.

Katika mchezo huo wa mwisho mabao ya Yanga yalifungwa na Maxi Nzengeli aliyefunga mawili wakati Kennedy Musonda, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz KI wakifunga moja kila mmoja wao huku la Simba la kufutia machozi likifungwa na Kibu Denis.

Rekodi zinaonyesha timu hizo zimekutana mara 60  Jumamosi katika Ligi Kuu Bara tangu zilipoanza kukutana mwaka 1965 huku Yanga ikiwa mbabe zaidi mbele ya Simba kwani imeshinda mara 25 na kupoteza 16 huku michezo 19 ikienda sare.
Katika michezo hiyo, yamefungwa jumla ya mabao 124 na Yanga imefunga 72 huku kwa upande wa watani zao Simba ikifunga 52.

Kichapo kikubwa kinachokumbukwa Jumamosi ni kile Yanga ilichoifunga Simba wakati ikifahamika kama Sunderland cha mabao 5-0, Juni 1, 1968 yaliyofungwa na Maulid Dilunga na Salehe Zimbwe waliofunga mawili kila mmoja na Kitwana Manara.

Hata hivyo hili ni pambano la 14 kwa timu hizo kukutana Aprili katika Ligi Kuu Bara tangu 1965 na katika mechi 13 zilizopita Simba imeshinda minne huku Yanga ikishinda mara tatu tu na michezo mingine sita iliyobakia ilimalizika sare. Kocha wa zamani wa Yanga na Singida Fountain Gate, Hans Van de Pluijm alisema mchezo baina ya miamba hiyo siku zote huwa hautabiriki kutokana na ugumu wake kwa sababu mtu mmoja anaweza kufanya jambo linaloweza kuleta faida au hasara kwenye timu.

“Huwa ni mchezo mkubwa na mgumu kwa kila timu ingawa ukiangalia kwa mwenendo wa Yanga kwa sasa unaweza kuipa ushindi japo ninachoamini atakayekuwa makini kwenye kutumia vizuri nafasi na kuepuka makosa ndiye atakayekuwa na faida zaidi.”