Joash Onyango, Mugalu kama kawa

Joash Onyango, Mugalu kama kawa

NYOTA wawili wa Simba beki, Joash Onyango aliyeumia kifundo cha chini mguu wa kulia na straika Chris Mugalu aliyeumia nyonga wamerejea mazoezini.

Kikosi hiko ambacho kinaendelea na mazoezi makali ya nguvu na mbinu katika Uwanja wa Mo Bunju Arena kuikabili Plateau United ya Nigeria kwenye mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Daktari wa Simba, Yassin Gembe alisema wachezaji wote wapo fiti na wanaendelea na mazoezi.

“Onyango yupo vizuri na alianza kufanya mazoezi na wenzake tangu Arusha kabla ya kufika hapa Dar es Salaam na hivyo hivyo kwa Mugalu ambaye tulikuwa nae Arusha katika kambi ya siku chache kabla ya kwenda Nigeria na kuhusu kutumika au kutokutumika hili ni jukumu la kocha mkuu ila kila mchezaji yupo tayari kwa mapambano,” alisema Gembe.

Magalu tangu amesajiliwa na Simba kabla ya msimu huu kuanza imeitumikia timu hiyo katika michezo saba ya mashindano yote na amefunga mabao saba.

Katika hatua nyingine kiungo fundi wa Simba, Mzambia Clatous Chama ameliambia Mwanaspoti kuwa amekuwa akifunga mabao muhimu katika michezo mbalimbali si kutokana na ujanja wake bali ni ushirikiano ambao anaupata kutoka kwa wachezaji wanzake ambao huusika kuandaa shambulizi.

Chama alisema ukiangalia bao ambalo aliwafunga Plateau United ugenini lilitokana na shambulizi ambalo, Luis Jose Miquissone ambaye aliwapiga chenga mabeki na kupiga krosi ambayo aliimalizia kwa kuweka mpira nyavuni.

“Kwangu nakuwa mchezaji wa mwisho wa Simba kuweka mpira nyavuni lakini ukweli nguvu na pongeza kubwa huanzia kwa wachezaji wenzangu ambao huusika kuandaa shambulizi ambalo linakwenda kuzaa bao,” alisema Chama ambaye amekuwa akiifungia timu hiyo mabao muhimu na katika mechi muhimu.

Miongoni mwa mechi muhimu ambazo Chama amefunga mabao muhimu ukiachana na hiyo ya Plateau United ambayo Simba imeweka rekodi kuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kupata ushindi Nigeria, amefunga dhidi ya Nkana Red Devils na AS Vita.

BY THOBIAS SEBASTIAN