JKU kiroho safi kwa Yanga SC

Muktasari:
- Katika mchezo huo wa fainali JKU iliyozing’oa Singida Black Stars na Azam, ilikubali kichapo cha bao 1-0 lililowekwa kimiani na Maxi Nzengeli na kuifanya Yanga kufikisha taji la saba ikiwa ndiyo klabu iliyotwaa mara nyingi ikiizidi Simba yenye sita likiwamo taji la msimu uliopita ilipouifunga Azam.
KOCHA wa timu ya JKU, Haji Ali Nuhu amekubali matokeo ya kulikosa taji la Muungano walililolipigia hesabu mapema, lakini akiwapongeza wachezaji wa timu hiyo kwa kujitoa na kuonyesha kiwango kizuri katika michuano hiyo iliyomaliizika juzi usuku kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.
Katika mchezo huo wa fainali JKU iliyozing’oa Singida Black Stars na Azam, ilikubali kichapo cha bao 1-0 lililowekwa kimiani na Maxi Nzengeli na kuifanya Yanga kufikisha taji la saba ikiwa ndiyo klabu iliyotwaa mara nyingi ikiizidi Simba yenye sita likiwamo taji la msimu uliopita ilipouifunga Azam.
Kocha aliliambia Mwanaspoti, licha ya kupoteza mchezo wa fainali dhidi ya Yanga, anajivunia wachezaji wake kutokana na namna walivyopambana kuanzia hatua za awali hadi fainali.
“Mashindano haya yametupa nafasi ya kujipima, pia nafurahishwa na nidhamu, ari na mbinu nzuri ambazo vijana wangu walizionyesha. Wameonyesha wana uwezo mkubwa,” alisema Nuhu.
JKU iliiondoa Singida Black Stars kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ya mabao 2-2 dakika 90, kabla ya kuitoa Azam FC kwa mabao 2-1.
Katika mchezo wa fainali, JKU ilikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Yanga SC, bao pekee lililofungwa na Max Nzengeli dakika ya 45 akiunganisha kwa ustadi pasi ya Farid Mussa.
Kocha huyo alisema mechi dhidi ya Yanga ilikuwa ya ushindani mkubwa na aliukubali muziki wa wapinzani wao ambao walionyesha ubora mkubwa wa kiufundi na uzoefu wa kimataifa.
“Yanga walitufunga kwa uwezo. Ni timu kubwa, ina wachezaji waliozoea mechi kubwa. Lakini tumejifunza mengi kutoka kwao na tutaenda kurekebisha makosa yetu,” aliongeza Nuhu.
Miongoni mwa nyota waliowika upande wa JKU ni Nizar Abubakar, kinda anayekipiga kwa mkopo kutoka Azam, ambaye alitajwa kuwa mchezaji bora chipukizi wa mashindano hayo.
Mashindano ya Muungano ya mwaka huu yameonekana kuongeza hamasa kisiwani Pemba, yakikutanisha timu kutoka Tanzania Bara na Visiwani na kuimarisha mshikamano wa michezo.