JIWE LA SIKU: Haya yanaweza kumtokea Diarra, Yanga ijipange

Muktasari:
- Kama Mali itavuka salama maana yake Inonga atakuwa na kazi ya kukabiliana na Diarra ikiwa ni miezi mitatu tu imepita tangu nyota hao wakutane kwenye Kariakoo Derby iliyopigwa Novemba 5, mwaka jana na Inonga na chama lake la Simba kutia aibu ya kufungwa mabao 5-1 na Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Beki wa Simba aliyepo na timu ya taifa ya Dr Congo, Henock Inonga keshamaliza kazi kwa kuandika historia ya Ligi Kuu Bara kupenyeza mtu kwenye nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) ikiwa ni kwa mara ya kwanza, baada ya timu hiyo usiku wa kuamkia leo kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Guinea.
DR Congo ilipata ushindi huo katika mechi ya robo fainali ya Afcon inayoendelea nchini Ivory Coast ikiungana na Nigeria iliyotangulia mapema baada ya kuifunga Angola kwa bao 1-0.
Inonga ambaye amekuwa panga pangua katika kikosi cha kwanza cha DR Congo kwenye michuano hiyo, kwa sasa anasikilizia matokeo ya mechi ya nusu fainali ya tatu inayopigwa usiku wa leo kuanzia saa 2:00 wakati Mali ya kipa wa Yanga, Djigui Diarra itakapowakabili wenyeji Ivory Coast.
Kama Mali itavuka salama maana yake Inonga atakuwa na kazi ya kukabiliana na Diarra ikiwa ni miezi mitatu tu imepita tangu nyota hao wakutane kwenye Kariakoo Derby iliyopigwa Novemba 5, mwaka jana na Inonga na chama lake la Simba kutia aibu ya kufungwa mabao 5-1 na Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Achana na Inonga, kwani kazi yake imeshamalizika baada ya ushindi wa kishindo dhidi ya Guinea, unaambiwa leo usiku kipa Diarra atazidi kuboresha rekodi ya kuwa kipa aliyedaka idadi kubwa ya mechi za Mali ikiwa atapangwa katika mchezo huo wa robo fainali dhidi ya wenyeji Ivory Coast utakaopigwa kwenye Uwanja wa La Paix, Bouake.
Hadi sasa, mechi 58 alizoitumikia Mali katika mashindano tofauti zimemfanya Diarra awe kipa anayeongoza kwa kuichezea nchi hiyo mara nyingi akimpiku aliyekuwa akishikilia rekodi hiyo, Ousmane Farota aliyeidaka katika mechi 57.
Lakini ukiweka kando hilo, kibarua kigumu kwa Diarra leo ni kuisaidia Mali kupata ushindi utakaoifanya timu hiyo kutinga kwa mara ya saba katika nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kufanya hivyo 1972, 1994, 2002, 2004, 2012 na 2013.
Mali inaingia katika mechi hiyo ikiwa na mwendelezo wa kufanya vyema katika mashindano hayo awamu hii ambapo hadi sasa haijapoteza mechi yoyote ikipata ushindi katika mechi mbili na kutoka sare mbili ambapo imefunga mabao matano na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili.
Mali katika mechi ya leo itamtegemea zaidi nyota wake Lassine Sinayoko katika kusaka mabao kutokana na uwezo wa kufunga aliouonyesha kwenye fainali hizo ambapo ameipatia mabao matatu huku Ivory Coast inaelekeza matumaini yake kwa Seko Fofana na Jean-Philippe Krasso ambao kila mmoja amefunga bao moja sawa na Franck Kessie.
YANAYOWEZA KUMTOKEA
Diarra hakuwa chaguo la kwanza kabla ya fainali hizi za 34 kule Ivory Coast, lakini tangu alipocheza mechi ya kwanza ya makundi ameendelea kuaminiwa langoni na kocha mkuu Eric Chelle na kufikia sasa ameruhusu mabao mawili katika mechi nne walizocheza.
Na leo kipa huyo wa Yanga ana nafasi ya kuwavuruga wenyeji Ivory Coast kwa kuwabania wasipate bao katika mechi itakayopigwa mapema saa 2:00 usiku, ambapo wenyeji walicheza kwa kiwango bora kisichotarajiwa na kuwaengua watetezi Senegal kwa matuta katika hatua ya 16-Bora.
Kama ataendelea na moto uleule alioanza nao kwenye fainali hizo, basi kuna uwezekano mkubwa wa kipa huyo kuzidi kujiweka sokoni kwa sababu tayari mawakala mbalimbali wa kimataifa wanaifuatilia michuano hiyo na huenda jina lake lipo kwenye mafaili ya jamaa hao.
Tayari inaelezwa kuna klabu za Afrika Magharibi zimekuwa zikimtolea macho kipa huyo wa Mali na kadri anavyozidi kufanya makubwa ndivyo anavyofungua milango ya kutakiwa na timu nyingine za nje.
YANGA IJIPANGE
Kufanya vyema kwa Diarra kunaweza pia kumuongezea thamani kubwa wakati huu akiendelea kuutumikia mkataba na klabu ya Yanga, kwani pale utakapoisha utaifanya Yanga iwe na kazi kubwa ya kumzuia asiondoke kwa dau kubwa na hapo atajineemesha kama bado anataka kuendelea kusalia Jangwani.
Kung'ara kwa Diarra kunazidi kumhakikisha namba ya kuwa kipa wa kwanza wa Yanga, kwani michuano hiyo ya Ivory Coast imezidi kutengeneza pengo kubwa baina yake na makipa wenzake waliosalia Metacha Mnata na Abuutwalib Mshery.
Mbali na kutoboka zaidi, lakini makali ya Diarra yanamuweka kwenye nafasi ya kuondoka klabuni iwapo watajitokeza matajiri wanaomhitaji, kitu kinachoweza kuwa kigumu kwa Yanga kumzuia kama ilivyotokea kwa straika Fiston Mayele.
Hata hivyo, Yanga haipaswi kuwa na presha kubwa kwa sababu kupanda thamani ya Diarra kwa sasa kunaweza kuzitia uoga timu nyingine kutaka kumnunua ambapo kwa mujibu wa mtandao wa Transfermarkt, thamani ya kipa huyo sokoni kwa sasa ni Euro 200,000 (zaidi ya Sh548 milioni).
Na jambo la tatu ambalo linaonekana linaipa Yanga uhakika wa kumbakiza Diarra ni ukaribu na uhusiano mzuri uliopo baina ya kipa huyo na uongozi pamoja na mashabiki, japo kocha wa makipa na mchezaji wa zamani wa Yanga, Juma Pondamali 'Mensah' amesema Yanga inapaswa kuhakikisha inambakiza Diarra kwa muda mrefu.
"Diarra ni kipa mzuri na kwa muda ambao amecheza katika ligi yetu ameonyesha kitu cha utofauti na makipa wengine. Tangu Yanga imemsajili amekuwa akitoa mchango mkubwa kwao hivyo kipa kama huyu sio wa kumuacha aondoke kirahisi," amesema Pondamali.
Kipa wa zamani wa Simba na Yanga, Ivo Mapunda aliwahi kumzungumzia Diarra akisema ni kipa anayetoa somo kwa makipa wazawa kwa namna ya uchezaji wake hasa wa kutumia miguu pamoja na kuanzisha mashambuliaji kuanzia langoni mwake, kitu ambacho kwa soka la kisasa ndicho kinachotakiwa na kuhitajiwa na makocgha wengi.
Kipa huyo tangu atue Yanga ameiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo, Kombe la ASFC mara mbili mfululizo na kutwaa Ngao ya Jamii mara mbili mbali na kuiwezesha Yanga kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kulikosa taji kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2 dhidi ya USM Algers ya Algeria naye kuchaguliwa kipa bora na Fiston Mayele kuwa Mfungaji Bora.