JIWE LA SIKU: Haina haja ya kupaniki, timu mbovu haichezi robo fainali CAF

Muktasari:

  • Kipigo cha juzi cha 2-1 kinafuatia kipigo cha 5-1 katika mechi ya duru la kwanza la ligi walichopata Wekundu wa Msimbazi kutoka kwa timu hiyo ya Wananchi.

SIMBA juzi imepoteza mechi ya pili ya Ligi Kuu Bara dhidi ya mahasimu wao msimu huu kwa jumla ya mabao 7-2 ikimuachia mtani pointi zote sita.

Kipigo cha juzi cha 2-1 kinafuatia kipigo cha 5-1 katika mechi ya duru la kwanza la ligi walichopata Wekundu wa Msimbazi kutoka kwa timu hiyo ya Wananchi.

Kwenye msimamo Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 46, ikizidiwa kwa pointi 12 na vinara Yanga ambao wanafukuzia taji lao la tatu mfululizo la Ligi Kuu Bara. Hata hivyo, Simba ina mechi moja mkononi ukilinganisha na Yanga iliyocheza mechi 22

Simba imezidiwa pointi 5 na Azam iliyo katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 51, lakini Simba imecheza mechi mbili pungufu ya wanalambalamba. Kama Simba ikishinda mechi zake za mkononi itafikisha pointi 52.

Takwimu hizo kwa ujumla haziwafurahishi mashabiki wa Simba. Zimekuwa zikiwapa nguvu wapinzani wao na watani wao kuwakebehi kwamba timu yao ni mbovu kiasi kwamba kelele nyingi zimeanza kuwachukua na mashabiki wa Simba nao kuungana na wale watani wao kusema: “Tatizo la Simba, timu yetu ni mbovu.”

Lakini ni kweli Simba ni mbovu? Timu mbovu inacheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika? Hili ni swali muhimu kujiuliza.

Simba msimu huu ilicheza robo fainali yake ya tano ya Afrika katika miaka sita, robo-fainali nne zikiwa ni za Ligi ya Mabingwa na moja ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mwaka huu Simba ilitolewa kwa jumla ya mabao 3-0 dhidi ya Al Ahly ya Misri, ikifungwa bao 1-0 nyumbani na kisha kwenda kulala 2-0 ugenini, Cairo.

Kipigo cha bao 1-0 Dar es Salaam kilikuwa ni cha kwanza kwa Simba kupata kutoka kwa Al Ahly kwenye ardhi ya nyumbani. Mashabiki wamekasirika kwa sababu rekodi ile ya kujivunia kwamba Simba ilikuwa haijawahi kufungwa na Al Ahly nyumbani sasa imefutika.

Mashabiki wa Simba wana hasira kwa sababu, Simba ndiyo timu pekee ambayo imefungwa nyumbani na ugenini kati ya timu zote 8 zilizocheza hatua ya robo fainali msimu huu.

Lakini Simba hii inayoonekana ni mbovu ndiyo timu ambayo katika mechi ya Dar es Salaam dhidi ya mabingwa mara 11 wa Afrika, Ahly, ilitawala mechi yote ikimiliki mpira kwa asilimia 63 dhidi ya 37 za wababe hao kutoka Misri.

Katika mechi hiyo ya Machi 29, 2024 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba ilipiga mashuti 19 dhidi ya matano tu ya Ahly, huku mashuti 7 ya Wekundu yakilenga lango. Shuti pekee la Ahly ambalo lililenga lango la Simba ndilo lililokuwa bao lililoamua mechi.

Simba ilipiga kona 11 dhidi ya kona 4 tu za Al Ahly.

Kiujumla Simba ilitawala kwa kila kitu mechi hii dhidi ya mabingwa watetezi wa Afrika.

Mwingine atakwambia “Waarabu wana kawaida ya kujilinda ugenini na kukuachia mpira ucheze wewe wakati wao wakitafuta matokeo tu.” Ni kweli. Lakini kujilinda hakuwi kwa staili ile dhidi ya Simba ambapo unapiga mashuti 19 langoni mwao na saba yanalenga lango.

Wanaojua staili ya kupaki basi wanatambua kuwa timu inayoamua kucheza kwa mtindo huo haikupi nafasi ya kupiga mashuti 19 langoni mwake yakiwamo saba ya kulenga lango. Timu ya kucheza staili hiyo haikuruhusu kumfikia wala kumkaribia kipa wao na mara nyingi kipa wa timu iliyopaki basi huwa “anasoma gazeti” (msemo wa utani wa mpirani pale kipa anapomaliza mechi bila ya kufanya ‘save’ yoyote ya maana au anapolazimishwa kuokoa mara chache sana).

Kwa wanaojua boli na staili ya kujilinda ukiwauliza watakwambia kuhusu hili, kwamba katika ile mechi Ahly walipotezwa vibaya sana na Simba na si kweli kwamba waliwaachia mpira waucheze Wekundu wa Msimbazi.

Tofauti pekee iliyokuwapo siku ile kwa Mkapa, ni kwamba Simba imekuwa ikishindwa kuzibadili nafasi nyingi inazotengeneza msimu huu kuwa mabao.

Kama timu inaweza kutawala mpira kwa asilimia 62 dhidi ya mabingwa watetezi wa Afrika, inawezekana vipi timu hiyo ikaitwa timu mbovu?

Hiyo sio timu mbovu. Ni timu ambayo ina udhaifu katika maeneo fulani ambayo, yanatakiwa kufanyiwa kazi ili mashuti yale saba yaliyolenga lango dhidi ya Al Ahly matatu yawe mabao. Ni hapo tu.

Ni makosa makubwa kuiita timu hii iliyoenda kutawala mchezo dhidi ya Al Ahly kule ugenini Cairo kuwa ni mbovu, licha ya kwamba ilifungwa mabao mawili.

Mpira ni saikolojia. Kama Simba ilipotawala mchezo hapa ingefunga mabao mawili ama matatu kutoka katika mashuti yale saba yaliyolenga lango, mechi ya marudiano kule ugenini ingekuwa tofauti kabisa.

Hii Simba inayoitwa mbovu imefungwa mabao 2-0 kule ugenini ambako ilitawala mchezo na ilitengeneza nafasi kadhaa za kufunga, lakini kulikuwa na timu ambayo mashabiki wengi wa Simba watakwambia ni kikosi bora kabisa cha Wekundu wa Msimbazi, lakini kilifungwa 5-0 kule Misri Februari 2, 2019. Ukiangalia haya unaweza kuona Simba hii sio mbovu bali kuna upungufu katika maeneo machache ambayo yakifanyiwa kazi timu itatisha sana na kubwa ni eneo la umaliziaji.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, Simba imeshika nafasi ya pili kwa kutengeneza nafasi nyingi (big chances created) ikipika nafasi 19, ikiwa nyuma ya Al Ahly pekee iliyotengeneza nafasi kubwa 24.

Simba pia imeongoza wastani wa kupiga mashuti mengi yaliyolenga lango kwa mechi za Ligi ya Mabingwa msimu huu ikiwa na wastani wa mashuti 4.4 (sawa na Yanga), zikiwa juu ya Mamelodi Sundowns iliyopiga wastani wa mashuti yaliyolenga lango (4.3).

Clatous Chama pia ameongoza kwenye kupika nafasi nyingi zaidi za hatari kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu akitengeneza nafasi 5 sawa na Stephane Aziz Ki wa Yanga wanaoongoza wakifuatiwa na Mohamed Chibi wa Pyramids FC (4).

Simba pia iliongoza kwa mabao katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa ikifunga mabao 9, sawa na Yanga, huku pia Simba ikishika nafasi ya tatu kati ya timu zilizoruhusu mabao machache zaidi katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Nafasi ambazo Simba ilitengeneza katika mechi dhidi ya Yanga jana, kama ingezitumia mechi ile ingekuwa na matokeo tofauti sana.

Kwa mfano katika mechi ile ya juzi, ni Simba ndiyo iliyopiga mashuti mengi zaidi ya waliyopiga Yanga.  Simba ilipiga mashuti 10, Yanga ilipiga mashuti 7. Kila timu mashuti yaliyolenga lango yalikuwa manne-manne, na yaliyoenda nje ya lango Simba ilipiga sita, Yanga matatu. Simba ilipiga kona 4, Yanga kona 3. Kwanini Simba ilipoteza mchezo wakati ilifanya majaribio mengi zaidi? Ni kweli hii timu ambayo inafanya majaribio mengi zaidi ndio timu mbovu?

Wengi watakwambia Simba ni mbovu kwa sababu ilifungwa 5-1 na Yanga katika duru la kwanza la msimu huu wa Ligi Kuu Bara. Lakini kufungwa mabao mengi katika mechi moja, sio lazima imaanishe kwamba timu iliyofungwa ni mbovu. Matokeo ya aina hiyo hutokea mara chache, na zaidi ni pale timu ‘inapojichanganya’ tu na ‘kuingia katika mfumo’ wa mpinzani inaweza kujikuta inaadhibiwa kwa mabao mengi. Kwani Simba ile iliyofungwa 5 duru la kwanza imebadilika nini cha maana hadi ikawa hii ambayo iliwafanya mashabiki wa Yanga waombee mechi iishe katika dakika zile za refa Ahmed Arajiga Jumamosi?

Simba inahitaji marekebisho machache zaidi katika umaliziaji ili kutisha tena. Na kwa kocha huyu wa mataji Abdelhack Benchikha, Simba haiko mbali na yale makali yake.