Jezi zazuia mechi ya USM Alger, Berkane

Muktasari:

  • Imeelezwa kuwa msafara wa RS Berkane ulipofika vyumbani ukakuta jezi ambazo hazina bendera ya Morocco na hivyo wakagoma kuingia uwanjani na baada ya majadiliano marefu wakaondoka uwanjani.

Mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (CAF Confederation Cup) kati ya USM Alger ya Algeria na RS Berkane ya Morocco haujafanyika baada ya wageni Berkane kuzikataa jezi walizozikuta kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakidai sio zao.

Awali, RS Berkane ilidai jezi zao zilizuiwa Uwanja wa Ndege walipowasili Algeria kisha wakawaambia hawataruhusiwa kuzitumia kwa kuwa zina Bendera ya Morocco, jambo ambalo lilipingwa huku wakidai wanataka kuendelea kuzitumia na kama itashindikana hawataingia uwanjani kitu ambacho kilitokea.

Imeelezwa kuwa msafara wa RS Berkane ulipofika vyumbani ukakuta jezi ambazo hazina bendera ya Morocco na hivyo wakagoma kuingia uwanjani na baada ya majadiliano marefu wakaondoka uwanjani.

Wadau wanasubiri maamuzi kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa kuwa Kidiplomasia Algeria na Morocco hazina uhusiano mzuri na hiyo inatajwa kuwa chanzo cha Algeria kukataa uwepo wa Bendera ya Morocco kwenye jezi.
Mchezo mwingine wa nusu fainali uliopigwa jana ulishuhudia Zamalek ya Misri ikitoka suluhu na Dreams FC ya Ghana.