Jezi mpya Simba we acha tu

Muktasari:
Hadi kufika majira ya saa 7 mchana, jezi hizo ambazo zimetambulishwa wiki tatu zilizopita katika tamasha la Simba Day, zilikauka kwa wafanyabiashara hao ambao hutundika jezi zao kwenye miti iliyopo pembezoni mwa barabara inayopita Uwanja huo jambo lililofanya waanze kuhaha kusaka nyingine za kuuza.
JEZI mpya za Simba zenye nembo ya SportPesa jana ziligeuka bidhaa adimu kwa kugombewa kwa wingi na mashabiki wa klabu hiyo hali iliyofanya zimalizike mapema kwa wafanyabiashara waliokuwa wakiziuza nje ya Uwanja wa Taifa.
Hadi kufika majira ya saa 7 mchana, jezi hizo ambazo zimetambulishwa wiki tatu zilizopita katika tamasha la Simba Day, zilikauka kwa wafanyabiashara hao ambao hutundika jezi zao kwenye miti iliyopo pembezoni mwa barabara inayopita Uwanja huo jambo lililofanya waanze kuhaha kusaka nyingine za kuuza.
Rajabu Ramadhan, mmoja wa wafanyabiasha wanaouza jezi na bidhaa nyingine kwa mashabiki, aliliambia gazeti hili kuwa biashara ya jezi hizo imeenda vizuri kutokana na mashabiki hao wa Simba kukoshwa na usajili ambao wameufanya msimu huu ambao umehusisha wachezaji mastaa.
"Mimi binafsi mzigo wangu umemalizika tangu saa tano na hapa unaponiona najaribu kutafuta mzigo mwingine wa jezi za aina hiyo kwa sababu mashabiki wanaonekana kuzihitaji zaidi kulinganisha na jezi za aina nyingine za Simba au hata zile za Yanga ambazo tunaziuza hapa.
Kiufupi ni kwamba wengi wao wanaonekana kuwa na uhakika na timu yao ndio maana unaona wananunua jezi hizi mpya kwa wingi hasa zile zenye majina ya wachezaji wao mastaa ambao wamewasajili katika kipindi cha dirisha la usajili. Na sio mimi tu, leo biashara ta aina hii ya jezi imekuwa nzuri kwetu sisi wauzaji."