Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jangwani pafurika mashabiki wa Simba, polisi waimarisha ulinzi

JANGWANI Pict

Muktasari:

  • Tangu saa saba mchana eneo hilo lilianza kujaa mashabiki waliovalia jezi nyekundu na nyeupe, wakiimba nyimbo za kusifia chama lao huku wakionyesha furaha ya kutwaa taji hilo.

MAELFU ya mashabiki wa Simba wamefurika eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam wakisubiri kwa hamu kuwasili kwa msafara wa timu hio unaosherehekea ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB, lililotwaliwa jana baada ya kuifunga Azam bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali uliochezwa Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba.

Tangu saa saba mchana eneo hilo lilianza kujaa mashabiki waliovalia jezi nyekundu na nyeupe, wakiimba nyimbo za kusifia chama lao huku wakionyesha furaha ya kutwaa taji hilo.

Wengi walieleza kuwa walichagua kusubiri Jangwani ili kuushuhudia msafara huo ukipita katika eneo ambalo pia ni sehemu yenye historia kubwa ya ushindani kati ya Simba na watani wao, Yanga.

Kutokana na uwepo wa ofisi za Yanga katika eneo hilo, vyombo vya ulinzi na usalama vimeimarisha doria kwa kuweka idadi kubwa ya askari kuhakikisha shughuli zinaendelea kwa utulivu na hakuna atakayesababisha vurugu au uharibifu wa mali.

JANGWA 01

Mbali na askari kutanda eneo lote, uzio wa muda umewekwa kuzunguka sehemu ya ofisi za Yanga ili kuzuia mashabiki kusogea karibu na eneo hilo huku biashara zikiendelea kulindwa dhidi ya usumbufu wowote unaoweza kujitokeza.

Awali, kulikuwa na vizuizi vya barabarani vilivyowekwa kuzuia magari kupita lakini baadaye viliondolewa na kubaki magari mawili ya polisi mwanzo na mwisho wa  barabara ya Jangwani yakisimamia usalama wa eneo hilo.

Kutokana na umati mkubwa wa mashabiki waliotapakaa barabarani, magari ya kawaida yameshindwa kupita katika eneo hilo huku mashabiki wakilitawala kwa kuimba nyimbo za Simba na kushangilia ubingwa walioutwaa.

Eneo ambalo jana lilikuwa kitovu cha sherehe za Yanga baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC, leo limegeuka kuwa makutano ya mashabiki wa Simba waliojazana wakisubiri kuupokea msafara wa mabingwa wa Kombe la CRDB.

JANGWA 02

Kadiri muda unavyokwenda, idadi ya mashabiki inaendelea kuongezeka huku makundi mengine yakimiminika kutoka maeneo mbalimbali ya jiji kuungana na wenzao Jangwani.

Mpaka sasa, msafara wa Simba ulikuwa bado haujafika Jangwani lakini shamrashamra zimeendelea kushika kasi huku mashabiki wakiamini watapata fursa ya kusherehekea ubingwa huo katika eneo ambalo limekuwa sehemu ya ushindani mkubwa kati ya vigogo hao wa soka la Tanzania.