Ajitoa fahamu kisa Simba, mashabiki wamlazimisha kutoka barabarani
Muktasari:
- Shabiki huyo, aliyekuwa kifua wazi, alionekana akijilaza katikati ya njia ya mabasi ya mwendo kasi huku magari mengine pamoja na pikipiki zikiendelea kupita katika maeneo ya karibu, hali iliyowatia hofu mashabiki wengine waliokuwa wakishuhudia tukio hilo.
SHABIKI mmoja wa Simba amekuwa kivutio katika eneo la Karume wakati msafara wa timu hiyo wa kusherehekea ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB ukisubiriwa kupita, baada ya kufanya vitendo vilivyohatarisha usalama wake.
Shabiki huyo, aliyekuwa kifua wazi, alionekana akijilaza katikati ya njia ya mabasi ya mwendo kasi huku magari mengine pamoja na pikipiki zikiendelea kupita katika maeneo ya karibu, hali iliyowatia hofu mashabiki wengine waliokuwa wakishuhudia tukio hilo.
Tukio hilo lilizua taharuki zaidi pale basi la mwendo kasi lilipokaribia eneo alilokuwa amelala, badala ya kuondoka, aliendelea kubaki barabarani huku akionekana kutokuwa na hofu yoyote.
Mashabiki wenzake waliinuka haraka na kumvuta pembeni ili kuzuia hatari yoyote ambayo ingeweza kujitokeza kabla hali haijawa mbaya zaidi.
Baadhi ya watu waliokuwa eneo hilo walidai shabiki huyo alionekana kuwa amelewa kabla ya kuanza kufanya vituko hivyo, jambo ambalo huenda lilichangia kuhatarisha maisha yake.
Licha ya shamrashamra za kusherehekea ubingwa huo, tukio hilo limeibua wito kwa mashabiki kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha yao au ya wengine wakati wa sherehe za aina hiyo.