Mashabiki wagusa Kombe, Simba yaliteka jiji kwa paredi la ubingwa
Muktasari:
- Kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Karume, Msimbazi na maeneo mengine ambayo msafara ulipita, mashabiki walijitokeza kwa wingi wakipeperusha bendera, kuimba nyimbo za kuisifu timu hiyo na kushangilia wachezaji pamoja na benchi la ufundi.
JIJI la Dar es Salaam limegeuka kuwa jekundu na jeupe baada ya maelfu ya mashabiki wa Simba kufurika katika mitaa mbalimbali kushuhudia paredi ya kusherehekea ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB, lililotwaliwa baada ya jana Jumamosi kuichapa Azam bao 1-0 kwenye fainali iliyochezwa Uwanja wa Gombani, Pemba.
Kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Karume, Msimbazi na maeneo mengine ambayo msafara ulipita, mashabiki walijitokeza kwa wingi wakipeperusha bendera, kuimba nyimbo za kuisifu timu hiyo na kushangilia wachezaji pamoja na benchi la ufundi.
Moja ya matukio yaliyoacha gumzo kwenye paredi hilo ni mashabiki kupewa nafasi ya kuligusa kombe la ubingwa lililokuwa mikononi mwa msemaji wa klabu, Ahmed Ally na wakati mwingine nahodha, Shomary Kapombe.
Kila gari liliposimama au kupunguza mwendo, Ahmed alilisogeza kombe pembeni ili mashabiki waliokuwa karibu waliguse huku wakishangilia kwa nguvu.
Simba ilikuwa na makombe yao yote mawili ikiwemo la Muungano ambalo walitwaa kwa kuichapa Yanga bao 1-0.
Wengi walionekana wakipiga picha na kurekodi video za tukio hilo kwa simu zao, huku wengine wakisema ni ndoto iliyotimia kuligusa kombe ambalo wamekuwa wakisubiri kuliona tena mikononi mwa timu hiyo.
Ushindi huo umeipa Simba sababu ya kumaliza msimu kwa tabasamu baada ya kukosa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC na kushindwa kufikia malengo katika baadhi ya mashindano mengine ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika ilipokwamia hatua ya makundi.
Kutwaa Kombe la CRDB kumeonekana kuwa zawadi kwa mashabiki walioendelea kuiunga mkono timu hiyo katika kipindi chote cha msimu.
Kombe hilo pia limefuta ukame wa miaka minne kwa Simba katika mashindano hayo, jambo lililoongeza thamani ya ushindi huo na kufanya shamrashamra za paredi kuwa za aina yake.
Katika maeneo mengi ambayo msafara ulipita, shughuli za kawaida zilisimama kwa muda huku wananchi wakikusanyika kandokando ya barabara kuwashuhudia mabingwa hao.
Baadhi walipanda majengo, vituo vya mabasi na sehemu za juu ili kupata nafasi nzuri ya kuuona msafara.
Wachezaji wa Simba walionekana wakifurahia mapokezi hayo kwa
kuwapungia mikono mashabiki, kuimba nao nyimbo za ushindi na mara kwa mara waliinua kombe kuonyesha mafanikio hayo kwa umati uliokuwa ukiendelea kuongezeka.
Kwa upande wa 'semaji', alionekana kuwa kiungo muhimu kati ya timu na mashabiki, akihakikisha kombe linawafikia mashabiki kwa kulisogeza karibu yao kila ilipopatikana nafasi salama ya kufanya hivyo, jambo lililoibua shangwe kubwa kila ilipotokea.
Paredi hilo linahitimisha wiki ya mafanikio kwa Simba na kuthibitisha ukubwa wa klabu hiyo kwa idadi ya mashabiki waliojitokeza kusherehekea taji hilo.