Ishu ya Fei toto na TFF ipo hivi

Muktasari:
- KIUNGO Feisal Salum ‘Fei Toto’ ameendelea kuisikilizia kamati ya Sheria na hadhi za wachezaji ya TFF ili kujua hatima juu ya kesi ya kimkataba baina yake na klabu ya Yanga.
KIUNGO Feisal Salum ‘Fei Toto’ ameendelea kuisikilizia kamati ya Sheria na hadhi za wachezaji ya TFF ili kujua hatima juu ya kesi ya kimkataba baina yake na klabu ya Yanga.
Yanga ilipeleka shauri kwenye kamati hiyo ikimtaka Feisal kutoa maelezo kwanini ameondoka ndani ya kikosi hicho na kuandika barua ya kuaga bila mazungumzo ya pande zote mbili na baada ya kusikilizwa Ijumaa iliyopita, TFF ilitoa barua iliyoeleza Feisal bado ni mchezaji wa Yanga kimkataba lakini ikifafanua kuwa uamuzi wa nini kifanyike kwa pande zote mbili utatolewa Jumatatu ya jana, ila hadi tunaingia mitamboni saa 1:00 usiku kulikuwa hakuna taarifa kamili huku baadhi ya viongozi waandamizi wa TFF wakisisitiza kwamba wahusika wa kesi hiyo watapatiwa hukumu zao kwa muda wao na si jambo la kuutangazia umma tena.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, Alex Mgongolwa alionekana kwenye ofisi za Shirikisho hilo lakini akatokomea ghafla na si yeye wala Katibu Mkuu wake Herman Kidufu waliopokea simu kutoa ufafanuzi.
Baada ya hapo tulimtafuta Ofisa Habari wa TFF, Mario Ndimbo na kuweka wazi hadi kufika saa 1 jioni alikuwa hajapokea barua yeyote kutoka kwa kamati husika.
Hapo awali, Mwanasheria wa Feisal, Nduruma Majembe alikiri kupokea barua ya TFF iliyothibitisha kiungo huyo kuwa bado mchezaji wa Yanga lakini aliweka wazi wanajipanga kwenda mbele zaidi kusaka haki.