Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wajumbe wagomea matokeo uchaguzi TOC, ulinzi waimarishwa

TOC Pict

Muktasari:

  • Uchaguzi huo uliahirishwa mara tatu kufuatia kuenguliwa kwa baadhi ya wagombea akiwamo Mtaka, kabla ya makubaliano ya TOC, Serikali na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) kuwarejesha wiki iliyopita na kuamuliwa ufanyike leo Julai 5, 2026.

Hali ya sintofahamu imeibuka kwenye uchaguzi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) baada ya mwenyekiti wa uchaguzi kutangaza matokeo yaliyogomewa na wajumbe.

Awali mchuano mkali  kwenye nafasi ya urais ulikuwa kwa Antony Mtaka,  mkuu wa mkoa wa Njombe na Henry Tandau aliyekuwa makamu mwenyekiti wa TOC.

Hata hivyo sintofahamu ilitokea baada ya Leonard Thadeo kutangazwa ndiye mshindi, huku zogo likisikika ndani ya chumba cha uchaguzi.

Wakati wa kutangaza matokeo, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Uchaguzi huo, Malangwe Mchungahela, aliwafukuza waandishi wa habari na kueleza kwamba mkutano huo ni wa wajumbe wa TOC huku polisi sita, wawili wakiwa na silaha za moto wakiimarisha ulinzi.

Waandishi wakiwa nje, Mkwawa na makamu wake, Maharagwe Mchungahela walitoka kwenye chumba cha mkutano na kuondoka, kabla ya wajumbe kuanza kupiga kelele wakidai kilichotangazwa si kile ambacho wao wamekichagua.

Wajumbe hao walitoka nje na kusimama vikundi vikundi, wakihoji uhalali wa Thadeo ambaye wakati wa kuhesabu kura alionekana kupata kura moja kutangazwa ndiye mshindi.

Waliokuwa mawakala wa wagombea walidai Thadeo alipata kura moja, Tandau kura saba na Mtaka kura 29, lakini wakati wa kutangaza imekuwa kinyume.

Mkwawa alipoulizwa na Mwananchi kuhusu matokeo hayo, alisema kuna simu ya muhimu anazungumza nayo na kutokomea kusikojulikana.

Huku ulinzi wa polisi wenye silaha za moto ukiwa umeimarishwa, baadhi ya viongozi wa TOC wanaomaliza muda wao nao waliondoka ambapo rais wa TOC anayemaliza muda wake, Gulam Rashid akishangaa kilichotokea.

"Nilitoka nje wakati matokeo yanatangazwa, mwanzo nilisikia Mtaka ndiye ameshinda, lakini nimerudi nasikia Thadeo ndiye ametangazwa, nini kimetokea?" Alihoji Gulam.

Thadeo baada ya matokeo kutangazwa alitoka nje ya ukumbi akiwa kama anaongea na simu na kutamka neno moja tu kwamba huo ndiyo uchaguzi na kuondoka eneo la tukio.

Baada ya sintofahamu hiyo, utaratibu wa kuapishwa washindi haukufanyika huku wajumbe wakikaa vikundi vikundi wakipinga matokeo hayo wakidai hawayatambui.

Walidai hawajawahi kuona uchaguzi wa aina hiyo na kudai kuna namna imefanyika.

Mwanamichezo wa zamani, Suleiman Nyambui amesema kilichofanyika ni uhuni.

"Thadeo wakati kura zinahesabiwa alishakubali matokeo na kukiri kura hazijatosha, sababu alipata kura moja tu, imekuwaje ndiye atangazwe mshindi?" Amehoji Nyambui.

Mpiga kura kutoka Zanzibar, Mohamed Salim amedai hawajakubaliana na matokeo yaliyotangazwa.

"Uchaguzi gani mshindi hajaapa, ametangazwa kisha kamati ikatokomea na yeye akaondoka, huu uchaguzi sisi kama wapiga kura hatujakubaliana na matokeo," amesema.

Uchaguzi huo uliahirishwa mara tatu kufuatia kuenguliwa kwa baadhi ya wagombea akiwamo Mtaka, kabla ya makubaliano ya TOC, Serikali na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) kuwarejesha wiki iliyopita na kuamuliwa ufanyike leo Julai 5, 2026.