Kocha wa Yanga atua AS FAR
Muktasari:
- AS FAR imefikia uamuzi huo baada ya kutoridhishwa na matokeo ya msimu wa 2025/26, ambapo Santos alishindwa kuiongoza timu kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, huku pia ikimaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu ya Morocco.
RABAT, MOROCCO: KLABU ya AS FAR ya Morocco imemtangaza rasmi aliyekuwa kocha wa Yanga, Mreno, Pedro Goncalves, kuwa Kocha Mkuu mpya wa timu hiyo, akichukua nafasi ya Alexandre Santos aliyeondolewa mwishoni mwa msimu uliopita.
AS FAR imefikia uamuzi huo baada ya kutoridhishwa na matokeo ya msimu wa 2025/26, ambapo Santos alishindwa kuiongoza timu kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, huku pia ikimaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu ya Morocco.
Kutokana na kushindwa kufikia malengo hayo, uongozi wa klabu hiyo umevunja ushirikiano na Santos na kumkabidhi Pedro Gonçalves mkataba wa miaka miwili wa kuiongoza timu hiyo.
Pedro anatua AS FAR akitokea Yanga, aliondoka baada ya mkataba wake kusitishwa na mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha huyo amepewa jukumu la kuijenga upya AS FAR na kuirejesha katika ushindani wa juu, baada ya timu hiyo kukosa nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na badala yake kujikatia tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.
Licha ya kushuka kucheza Kombe la Shirikisho, AS FAR inaendelea kuwa moja ya klabu kubwa nchini Morocco ikiwa na kikosi chenye ubora, miundombinu ya kisasa na matarajio makubwa ya kurejea kwenye ushindani wa mataji ya ndani na kimataifa.
Kwa Pedro Gonçalves, kazi hiyo ni fursa mpya ya kuthibitisha uwezo wake katika moja ya ligi zenye ushindani mkubwa barani Afrika, huku akitarajiwa kuiongoza AS FAR kurejesha hadhi yake miongoni mwa vigogo wa soka la Afrika.