Inonga, Outtara waingia mtegoni Simba

BAADA ya kupoteza mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, wachezaji wa Simba hawakuwa na mapumziko kwani siku iliyofuata walianza mazoezi ya kuikabili Geita Gold kwenye mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa kesho Jumatano, Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Baaadhi ya mashabiki wamekuwa wakihoji kukaa benchi kwa mastaa akiwemo Shomari Kapombe na Joash Onyango kwenye ulinzi. Dhidi ya Yanga kwenye beki wa kati alicheza Henock Inonga pamoja na Mohammed Outtara ambao walionekana kutokuwa na mawasiliano mazuri kwani wote wamezoea beki namba nne huku nafasi ya Kapombe ikichukuliwa na Israel Mwendwa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Zoran alikiri mabeki hao wa kati (Inonga na Outtara) walifanya makosa ya kiulinzi kushindwa kukaba vizuri, ameliona hilo na kuna mabadiliko makubwa ya kiuchezaji yanakuja.
Alisema katika mazoezi ya wakati huu kabla ya kucheza na Geita kwenye mchezo wa kwanza wa ligi wanalifanyia kazi hilo ili kuona mabadiliko lakini anapambana kuwaweka vizuri kisaikolojia kusahau matokeo ya nyuma ili kupokea mbinu sahihi na vitu vya kufanya.
“Katika eneo la beki wa kati kuna ushindani wa kutosha ila mazoezi ndio yanaweza kuamua kama Inonga na Outtara wanaweza kurudi kikosi cha kwanza au akacheza Joash Onyango, Kennedy Juma au Erasto Nyoni,” alisema Zoran na kuongeza; “Wachezaji nilionao kila mmoja kwa nafasi yake akipambana na kujitoa kama majukumu yake yalivyo naamini watafanya vizuri, ingawa moja ya lengo letu kuchukua taji ya Ngao ya Jamii kushindwa kulifikia limetuuma.”
“Tunatakiwa kupambana ili kurudisha furaha kwa mashabiki wetu na hilo linawezekana tunaenda kupambana ili kuhakikisha tunafikia malengo yetu katika mashindano ya ndani yaliyobaki pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika, pia kutocheza kwa baadhi ya wachezaji ni kwasababu hawakuwa fiti.” alisema Zoran.