Ibenge awatega mastaa Azam, afichua usajili atakaoufanya

Muktasari:
- Ibenge amefunguka hayo muda mchache baada ya kusaini mkataba wa kuitumikia klabu hiyo, huku akiweka wazi anaenda kukaa na wachezaji ili waelewe nini anakitaka bila kujali atatumia mfumo gani.
KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge amesema atafanya usajili itakapohitajika, lakini anaamini kikosi kilichopo ni bora kutokana na kumaliza nafasi ya tatu na kupata nafasi ya ushiriki michuano ya kimataifa.
Ibenge amefunguka hayo muda mchache baada ya kusaini mkataba wa kuitumikia klabu hiyo, huku akiweka wazi anaenda kukaa na wachezaji ili waelewe nini anakitaka bila kujali atatumia mfumo gani.
“Kama Azam imemaliza nafasi ya tatu, ni wazi ina timu bora lakini kuna wachezaji wanatoka hivyo kama kutakuwa na umuhimu tutaingiza wengine, ila nguvu kubwa ni kuwa na nyota waliofanya makubwa,” amesema Ibenge raia wa DR Congo na kuongeza;
“Siwezi kupambana peke yangu, naomba ushirikiano kutoka kwa wachezaji, viongozi na mashabiki ili niweze kuipambania timu hii iweze kufikia malengo kupambana peke yangu sitaweza.”
Ibenge amesema anapenda kucheza mpira mzuri, lakini anapenda kushinda mechi na mataji, hivyo mashabiki watarajie mambo mazuri kutoka kwake.
Akizungumzia kuhusu ni mfumo gani rafiki atakaoutumia Ibenge amesema hawezi kuweka wazi, ila anaamini akikaa na wachezaji kwa muda wakimuelewa kila kitu kitakuwa wazi kwenye uwanja wa mechi.