Huu ndio udhaifu wa Fountain Gate, KenGold

Muktasari:
- Timu hiyo yenye maskani yake Babati mkoani Manyara katika kuruhusu nyavu zake kutikiswa imepishana bao moja tu na KenGold ambayo tayari imeshuka daraja ikiwa na mechi tatu za kucheza.
UKIANGALIA takwimu za Ligi Kuu Bara msimu huu utagundua kwamba Fountain Gate ndiyo timu nyepesi zaidi kuruhusu mabao iwe uwanja wa nyumbani au ugenini.
Timu hiyo yenye maskani yake Babati mkoani Manyara katika kuruhusu nyavu zake kutikiswa imepishana bao moja tu na KenGold ambayo tayari imeshuka daraja ikiwa na mechi tatu za kucheza.
Kwa sasa Fountain Gate iliyocheza mechi 27 imeruhusu mabao mengi zaidi ambayo ni 51 huku KenGold ikiruhusu 50.

Katika uwanja wa nyumbani wa Tanzanite Kwaraa, Fountain Gate imecheza mechi 14 kati ya 15 ikiwa tayari imeruhusu mabao 23 yakiwa ni mengi zaidi ikifuatiwa na KenGold (19).
Pia Fountain Gate imeruhusu mabao 28, ikiwa nafasi ya pili kwa timu zilizoruhusu nyavu zao kutikiswa zaidi ugenini wakati kinara ni KenGold (31).
Tatizo la kuruhusu mabao limekuwa changamoto kubwa kwa Fountain Gate ambayo hapo awali aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mohamed Muya aliwahi kunukuliwa akisema amekuwa akifanya mazungumzo mara kwa mara na safu yake ya ulinzi kuondoa tatizo hilo lakini ilikuwa ngumu.
Hivi karibuni, Kocha Robert Matano ambaye inaelezwa amewekwa kando kikosini hapo, alisema: “Timu ina makosa mengi ya safu ya ulinzi, kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha yanapunguza, bora timu isifunge lakini pia isiruhusu mabao.
“Tumekuwa tukifungwa zaidi ya kufunga, hili ni tatizo kubwa, lakini bado kuna nafasi ya kufanya vizuri kwenye mechi zilizobaki.”
Katika mechi 27 za Ligi Kuu Bara ilizocheza Fountain Gate msimu huu, ni tatu pekee dhidi ya Namungo (Agosti 29, 2024), Tabora United (Februari 17, 2025) na Tanzania Prisons (Februari 26, 2025) ambazo timu hiyo haijaruhusu bao msimu huu huku 24 zote nyavu zao zikitikiswa.
Mzigo huo wa mabao unawaangukia walinzi wa Fountain Gate ambao wamekuwa wakicheza mara kwa mara ni Anack Mtambi, Shafik Batambuze, Amos Kadikilo, Shaban Pandu, Jackson Shiga na Laurian Makame. Pia kipa namba moja wa kikosi hicho, John Noble ambaye amesimamishwa akiwa tayari amecheza mechi 16.
Ukiweka kando katika kuruhusu mabao, Namungo ndiyo timu iliyopoteza mechi nyingi nyumbani ambazo ni sita kati ya 13, ikifuatiwa na KenGold, Fountain Gate, Kagera Sugar, Tanzania Prisons na KMC ambazo kila moja mechi tano.
JKT Tanzania inatembea njia moja na Yanga kwa timu zilizopoteza mechi chache nyumbani ambazo ni mbili, kama ilivyo Singida Black Stars, wakati Simba imepoteza moja pekee.
Simba na Yanga ndiyo timu ambazo hazijapoteza viwanja vya ugenini, huku KenGold ikiongoza kwa kupoteza mechi 12 ikifuatiwa na Kagera Sugar (10).
Timu ambazo hadi sasa hazijashinda ugenini ni KenGold, Kagera Sugar, Dodoma Jiji na Coastal Union.